Tulieni, AS Vita Wanakufa Nyingi





KATIKA kuhakikisha hataki utani huku akitaka kuona timu yake inaibuka na ushindi wa mabao mengi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes amewatenga washambuliaji wake, Mkongomani, Chris Mugali na John Bocco na kuwapa program maalum ya kufunga mabao.

 

Simba inatarajiwa kuvaana na AS Vita katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa keshokutwa Jumamosi saa kumi kamili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.Bocco na Mugalu walipewa program maalum ya jinsi ya kufunga mabao pekee muda mfupi baada ya kumalizika kwa mazoezi ya jumla ya kikosi cha timu hiyo.

 

Katika mazoezi hayo yaliyofanyika Simba Mo Arena, Bunju, Dar, juzi Jumanne saa kumi kamili jioni huku yakishuhudiwa na Spoti Xtra, kocha huyo alimtaka kila mshambuliaji apige shuti au kumchambua huku akiwatengea kila mmoja mipira kumi kwa ajili ya kupiga golini na kufunga.

 

Gomes aliwatengea mipira hiyo nje ya 18 na kuwataka kupiga golini kwa ajili ya kufunga na lengo likiwa ni kuwaongezea umakini wanapofika katika eneo la hatari la wapinzani wakiwa katika maandalizi ya mchezo dhidi ya AS Vita.

 

Kocha huyo alitumia program hiyo kwa zaidi ya dakika 15 kwa kila mmoja kupiga mashuti 10 kwa kubadilishana huku golikipa akiwa Beno Kakolanya.Program hiyo iliwataka mastaa hao kupiga mashuti kwa kubadilisha miguu, kulia na kushoto, kabla ya baadaye kuwaongezea program ya kupiga mipira kwa kichwa.

 

Mipira hiyo ya vichwa ilikuwa inapigwa kutokea pembeni na kiungo mshambuliaji raia wa Kenya, Francis Kahata ambayo kati ya hiyo Bocco alifunga bao moja, huku mingine tisa ikiishia mikononi mwa Kakolanya.

 

Kwa upande wa Mugalu, hakufanikiwa kufunga.Akizungumzia kuhusu safu yake ya ushambuliaji, Gomes alisema: “Safu yangu ya ulinzi imekuwa ikifanya vizuri sana lakini safu yangu ya ushambuliaji imekuwa inashindwa kutumia kwa ufasaha nafasi tunazotengeneza, jambo ambalo ni lazima tulifanyie kazi.

“Mchezo wetu dhidi ya AS Vita ni muhimu kupata ushindi mzuri wa mbao mengi tukiwa katika uwanja wa nyumbani, kikubwa tunataka kumaliza tukiwa kileleni katika kundi letu.”

WAANDISHI: WILBERT MOLANDI, JOEL THOMAS NA MUSA MATEJA

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad