NI kufuru ya matumizi ya fedha, ndivyo unavyoweza kusema kufuatia kile ambacho Klabu ya Simba inaendelea kukifanya huko nchini Misri kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaopigwa kesho Ijumaa.
Simba iliyoondoka Dar juzi Jumanne kupitia Dubai wakielekea Cairo, Misri, muda mfupi kabla ya kuanza safari hiyo, walitoa taarifa wakisema: “Shukrani kwa Kampuni ya Ndege ya Emirates kwa ushirikiano ambao wametupatia wa kusafiri kutoka Dar es Salaam, Tanzania kwenda Cairo, Misri kwa kupitia Dubai.”Shirika hilo la ndege ni la Waarabu ambapo limewasaidia Simba kufika Cairo salama kwenda kuiua Al Ahly.
Kuelekea mchezo huo utakaopigwa katika Dimba la Kimataifa la Cairo, Simba imeendelea kuonesha umwamba wa fedha baada ya kufikia katika Hoteli ya Kitalii ya nyota tano inayotambulika kwa jina la Radisson Blu.
Hoteli hiyo inayopatikana katika Wilaya ya Heliopolis ndani ya Jiji la Cairo, inatoa huduma mbalimbali ikiwemo kifungua kinywa bure, vyumba vya hoteli vilivyodizainiwa vizuri na kuwekwa samani za kisasa ili kumpa mapumziko mwanana mgeni.
Pia kuna huduma ya masaji, baa, mgahawa wenye huduma za vyakula vya mataifa mbalimbali na bwawa la kuogelea.
Huduma nyingine ni pamoja na televisheni, WiFi katika kila chumba ambapo gharama ya chini kabisa ya chumba kuanzia ni Sh 162,222 huku ile ya juu zaidi ikiwa ni Sh 416,643 kwa usiku mmoja.
Chanzo chetu cha kuaminika kutoka ndani ya kambi hiyo, kimeliambia Spoti Xtra kwamba, baada ya timu kufika ndani ya hoteli hiyo jana Jumatano, kila mchezaji alipewa chumba chake ambapo wachezaji waliosafiri ni 26.Jumla msafara huo una watu 55 wakiwemo viongozi wa timu na wa benchi la ufundi.
Hivyo kwa idadi hiyo ya watu waliokuwa kwenye msafara huo na gharama za chumba kwa usiku mmoja, Simba inateketeza shilingi milioni 8.9 kwa siku, hivyo kwa siku tatu ambazo wanatarajia kuwepo Cairo kuanzia jana hadi kesho watakapolala kabla ya kuanza safari ya kurudi Jumamosi, watakuwa wameteketeza takribani Sh milioni 26,656,685 kwa kulala tu.
Hoteli hiyo pia inatoa huduma ya kusafirisha wageni wanaohitaji kutembelea Pyramid za Giza ambazo ziko umbali wa dakika 30 tu kwa mwendo wa gari kutoka hapo.Pia ipo huduma ya usafiri wa kuwarejesha wageni kutoka hotelini na kuwapeleka Uwanja wa Ndege wa Cairo ambao upo umbali wa kilomita tatu.
Vyumba vya hoteli hiyo vimewekwa hatika madaraja matano ambayo ni; Superior, Executive, Junior Suite, Executive Suite na Diplomatic Suite ambapo kila chumba na gharama yake.Simba inakamilisha ratiba tu ya hatua hiyo ya makundi kwani tayari imefuzu robo fainali ikiwa kinara wa Kundi A ikikusanya pointi 13, ikifuatiwa na Al Ahly yenye point inane ikiwa nafasi ya pili.
STORI: JOEL THOMAS NA CAREEN OSCAR, Dar