Waasi nchini Chad wametishia kumng’oa madarakani mtoto wa Rais aliyeuawa baada ya kuteuliwa kuwa kiongozi wa mpito nchini humo.
Kundi la waasi ambalo jeshi limelilaumu kwa mauaji ya Rais Idriss Deby Itno, limesema kuwa wapiganaji wake wanaelekea katika mji mkuu wa N’Djamena wakati huu. Waasi hao wanaojulikana kama “Front for Change and Concord”, wamesema katika taarifa kuwa Chad sio nchi ya kifalme.
Hali ya wasiwasi ilitanda mapema jana Jumatano juu ya umbali wa kiasi gani waasi hao watakuwa wameukaribia mji mkuu wa N’Djamena, mji wenye idadi ya watu milioni 1, na iwapo jeshi lingeendelea kuwa tiifu kwa Mahamat Deby baada ya kifo cha baba yake aliyedumu madarakani kwa miongo mitatu.
Haijabainika wazi walikofika waasi hao, japo taarifa za ujio wao zimezua hofu katika mji wa N’Djamena, ambao uliwahi kushambuliwa na kundi lengine la waasi mnamo mwaka 2008.Maafisa wa baraza la kijeshi wamesema mapambano ya kuwania udhibiti wa nchi bado hajakwisha.