Kocha wa AS Vita Florent Ibenge amekiri kuwa kwasasa vilabu vya Tanzania vimeimarika kifedha ndio maana vinaweza kusajili wachezaji kutoka DR Congo kwenye vilabu vikubwa kama TP Mazembe na AS Vita.
Kauli hiyo ameitoa baada ya hizo za DRC kuondolewa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku Simba SC ya Tanzania ikifuzu robo fainali kwa kuongoza kundi A.
''Mpira wa sasa unahitaji pesa, na kwa sasa vilabu vya Tanzania vipo vizuri kwenye pesa ndio maana vinamudu kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa. Hata wachezaji wa DR Congo wenye viwango vya juu wanakimbilia Tanzania,'' amesema Ibenge.
Simba imefuzu robo fainali baada ya jana April 3, 2021 kuifunga AS Vita magoli 4-1 na kufikisha pointi 13 na kuongoza Kundi A lenye timu za Al Ahly, AS Vita na Al-Merrikh.
Mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika TP Mazembe nao pia wameondolewa katika hatua ya makundi.