WAKATIaliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji akitajwa kurejea kwenye klabu hiyo, wachezaji wa zamani wa timu hiyo wamefunguka kuhusiana na ujio wake.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu taarifa zisambae za ujio wa bosi huyo aliyeifanyia Yanga mengi makubwa kipindi cha utawala wake akiwa mwenyekiti.
Manji amezua hofu kwa mashabiki wa Simba kutokana na ujio wake huku akiwa na rekodi kubwa ya kuchukua ubingwa mara tatu mfululizo 2014–15, 2015–16 na 2016–17.
Akizungumza na Championi Jumamosi, nahodha wa zamani wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema kuwa, kwake amezipokea kwa furaha taarifa za ujio wa Manji ndani ya Yanga.
Cannavaro alisema kuwa lipo wazi kati ya viongozi waliopita kuiongoza timu hiyo, Manji ni mmoja wapo kutokana na utawala bora aliokuwa nao.
“Hizo taarifa sidhani kama ni kweli, kama ni kweli basi ninaamini ile Yanga ya vikombe inakuja katika misimu ijayo na hilo linawezekana kwake.
“Manji alitengeneza kikosi bora kilichochukua ubingwa wa ligi mara tatu mfululizo na Ngao ya Jamii katika utawala wake tukiwafunga Azam FC pale Uwanja wa Mkapa.
“Na mafanikio yake yametokana na usajili bora aliokuwa anaufanya katika timu, kiukweli taarifa hizo nimezipokea kwa mikono miwili na leo (jana) usiku nitampigia simu kuthibitisha hilo kwani namba yake ninayo,” alisema Cannavaro.
Alipotafutwa kiungo wa zamani wa timu hiyo, Athumani Idd ‘Chuji’ kuzungumzia hilo, alisema kuwa: “Kwangu naona faraja kubwa kwa Wanayanga waliokuwa wenye ndoto za timu yao kuchukua ubingwa.
“Sijajua lini anakuja huyo Manji, lakini kwa mimi ninayemjua basi Wanayanga watarajie kuona usajili bora wa kisasa ukifanyika utakaoendana na hadhi ya Yanga.
“Mimi ninamfahamu vizuri Manji, kwani katika utawala wake nilikuwa sehemu ya wachezaji tegemeo, vitu vyake alikuwa akifanya kwa uwazi na siyo mgumu kutoa fedha yoyote ya usajili ili afanikishe usajili pamoja kambi nzuri.
”Naye mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Chinga One’ alisema kuwa: “Sijajua Manji atakuja kukaa nafasi gani, uongozi, mwanachama au vipi, lakini kwangu ninamkaribisha Yanga.“Ninaamini kama akija ataungana na wadhamini wengine katika kufanikisha mengi mazuri, hakuna asiyemjua Manji kutokana na kukumbukwa na mengi.”
STORI: WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam