Mbwa ni mnyama ambaye amekuwa akitumiwa na binadamu kwa muda mrefu kwa ajili ya ulinzi katika maeneo mbalimbali, ikiwamo majumbani. Ni mnyama ambaye amekuwa akitumia nyama kama chakula chake kikuu.
Pamoja na kuwa na sifa hizo, miaka ya zamani mnyama huyo alikuwa akitumiwa kama kitoweo na kabila moja maarufu hapa nchini.
Hata hivyo, mkoani Morogoro suala la mbwa kuwa kitoweo ni jambo geni na si utamaduni wa makabila yaliyopo mkoani hapa kutumia nyama ya mbwa kama chakula ama kitoweo.
Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro wamelaani vikali kitendo cha baadhi ya wauza mishikaki ndani ya manispaa hiyo kutumia nyama ya mbwa kama mishikaki na kuiomba Serikali kufanya uchunguzi ili kuwabaini wauzaji hao, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria.
Kuonyesha ukweli wa madai yao, Aprili 26, 2021 katika daraja kuu la barabara iendayo Iringa eneo la Relini, wananchi waliokuwa wakipita njia waliwakuta vijana watatu wanaodaiwa ni wauzaji mishikaki nje ya kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Msamvu Morogoro wakiwa wanachuna ngozi ya mbwa.
Walisema waliwaona vijana hao wakichuna mnyama lakini hawakujua kama ni mbwa, kilichowashtua ni pale walipoona pembeni kichwa cha mbwa, ndipo walipowafuata na wao kuonyesha mashaka, waliwakamata na kuwahoji na baadaye kuwapeleka kituo cha Polisi Msamvu, na baadaye watuhumiwa hao kuhamishiwa kituo kikuu cha Polisi Morogoro.
Mkazi wa Mafisa, Anold Alexanda alisema ni jambo la kushangaza kukuta wauza mishikaki wakitenda jambo hilo, kwani wanaondoa imani ya watu kuendelea kula nyama maeneo ya Msamvu.
“Hawa watu wanafahamika kwa uuzaji wa mishikaki hasa majira ya usiku, ndio wamekuwa wakiuza mara nyingi, unawakuta pale Puma kituo cha mafuta na Dodoma stendi. Watu tunakula na wanatuuzia mishkaki bila hata kujua kama ni ya mbwa ama la,” alisema Alexanda.
“Mimi ni mtumiaji mkubwa wa mishikaki na nimekuwa nikienda mara kwa mara wanapouzia, kiukweli wamenihuzunisha, ninachoomba hatua kali zichukuliwe dhidi yao,” aliongeza.
Dereva wa bodaboda eneo la Msamvu ndani, Abdallah Pawa alisema kwa tukio hilo, Serikali iwachukulie hatua kwa kuwalisha watu nyama za mbwa bila ridhaa yao. Aliwashauri wauza chakula katika maeneo mbalimbali manispaa ya Morogoro kuwa makini, waaminifu na maeneo wanayonunua nyama waepukane na nyama za kununua mitaani katika sehemu zisizofahamika.
“Tumesikia mmoja wao hao vijana ni wakala mkubwa wa wauza nyama za mishikaki hasa ya ile ya mia mia, kinachotakiwa ni kuepuka nyama za kununua mitaani, sio kila nyama unayoletewa unanunua, unatakiwa kuchukua nyama sehemu sahihi ukijua hii ni nyama ya mnyama fulani,” alisema.
Mfanyakazi wa stendi ya Msamvu, Samson Jonas alisema: “Idadi ya watu wanaoingia na kutoka hapa Msamvu ni wengi, huyu jamaa ni muuaji na atafanya wale wafanyabiashara wa mishikaki kukosa wateja, kwani si wote wanaouza nyama ya mbwa, wapo wanaouza mishikaki ya ng’ombe, mbuzi ama kuku.
“Hata sasa ukienda buchani lazima uangalie kwato kama nyama iliyopo ni mbuzi, ng’ombe ili ununue, sasa hivi watu wameshtuka, huyu jamaa katuumiza sana kiukweli,” aliongeza Jonas.
Muuza chipsi Mussa Said maarufu kama dokta Shiba alisema ameumia kama mfanyabishara kwa taarifa hiyo, na kuwataka wateja kuondokana na hofu hiyo kwani chakula kinachouzwa ndani ya kituo cha mabasi Msamvu ni salama. Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Fotunatus Muslimu alipoulizwa juu ya kuwepo kwa tukio hilo, alikiri kukamatwa kwa watuhumiwa watatu na kwamba wanafanyiwa mahojiano.
Waliokamatwa kutokana na tuhuma hizo za kukutwa wakichuna ngozi ya mbwa na kudai kuwa ni wauzaji mishikaki ni Hamza Rajabu (20), Omary Mohamed (12) wote wakazi wa Msamvu na Mussa Juma (30) mkazi wa Mtawala.