KIWANGO bora kinachooneshwa na mlinda mlango namba moja wa Simba, Aishi Manula, kimezidi kuwavutia wababe wengi wa soka ndani ya Afrika wakitaka saini yake.Manula ambaye msimu huu amefanya kazi kubwa hasa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, awali alikuwa akifukuziwa kwa ukaribu na Waarabu kutoka Sudan, Al Merrikh.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema kwamba, baada ya Al Merrikh kutangaza dau la zaidi ya Sh milioni 230 na mshahara wa Sh milioni 18 ili kumpata kipa huyo, sasa Wasauz nao wameingilia kati.
Mtoa taarifa huyo amelieleza Spoti Xtra kwamba, Wasauz hao ni Mamelodi Sundowns ambao ni vinara wa Kundi B katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.Aliendelea kufafanua kuwa, Mamelodi wameonesha nia ya dhati kutaka saini ya Manula ili kwenda kuwa mbadala sahihi wa kipa Mganda, Denis Onyango mwenye umri wa miaka 35 ambaye anatarajiwa kustaafu hivi karibuni.“
Achana na lile dili la Al Merrikh ambalo ni wazi Kocha Didier Gomes aligomea kutokana na kuwa na mipango na Manula huku akisema anaifahamu klabu hiyo haipo vizuri kiuchumi, kwa sasa Manula anatakiwa na Mamelodi.
“Mamelodi wamefi kia uamuzi huo baada ya Onyango kuwaambia anataka kustaafu, hivyo wakaangalia kipa gani kwa sasa ana uzoefu na michuano ya kimataifa halafu bado kijana atakayedumu kwa muda mrefu, wakaona Manula anawafaa. Wakaanza mchakato.“
Kwa ufupi wana ofa nzuri ambayo sidhani kama Simba watakataa,” kilisema chanzo hicho.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, alizungumzia usajili wa Manula akisema: “Hatuwezi kumzuia mchezaji kuondoka, kinachotakiwa ni kufuata tu utaratibu kwa wanaomtaka, walete ofa, tuone kama inatufaa na mchezaji akikubali basi tunamruhusu.
“Unajua sisi Simba hatuzuii mchezaji kuondoka, haya ni maisha yao, tupo tayari kumruhusu yeyote kuondoka lakini lazima taratibu zifuatwe.”
MUSA MATEJA