Na Amiri Kilagalila,Njombe
Jeshi la polisi mkoani Njombe linawashikilia watu tisa wa mtaa wa Itulike kata ya Ramadhani mjini Njombe kwa tuhuma za kutekeleza mauji ya Mme na Mke huku sababu kubwa ikitajwa kuwa mauaji hayo yametokana na imani za kishirikina.
Akizungumza na vyombo vya habari,kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Hamis Issah,amesema familia iliyouawa kwa nyakati tofauti kwa kupishana siku moja ni Nikodemas Ng’ande (60) mwanaume pamoja na Renatha Mtega (60) mwanamke wote wakazi wa Itulike.
“Tukio hili ni la kusikitisha wameuawa mke na mume,wameuawa kwa kupishana siku moja katika kijiji cha Itulike kata ya ramadhani.tarehe 19 mwezi wa 3 mwaka huu aliuawa mama Renatha Henry Mtega na maiti yake ikaenda kutupwa kwenye msitu wa TANWAT msitu huu ni wakupandwa miti aina ya paini”alisema Kamanda Hamis
Amemtaja marehemu mwingine kuwa ni Nikodemas Ng’ande “Tarehe ishirini akauawa mme wake naye akabebwa kutoka Itulike akapelekwa Maheve na mwili ulihifadhiwa hapo ukiwa umefungwa kwenye turbai”alisema Kamanda Issa
Kamanda Issah amesema taarifa za mauaji hayo zilipatikana mara baada ya mtoto wa marehemu Bwana Emmanuel Danford alipofika nyumbani kwao na kukuta nyumba tupu bila mtu yeyote hatua iliyomlazimu kuanza kutoa taarifa kwenye uongozi wa eneo husika.
Aidha amesema jeshi hilo limewakamata watu tisa kwa tuhuma za kukaa na kutengeneza mpango wa mauaji ya familia hiyo.
“Polisi ilianza kufanya uchunguzi na kukamata watu 9 ambao walikaa katika mahabusu ya polisi na baadaye katika uchunguzi ilibainika kuwa ndio walio kaa na kupanga kuua hawa watu wa familia moja na matokeo yake tarehe ya jana waliweza kwenda kuonyesha mwili wa marehemu mzee Nicodemas akiwa amekufa kikatili” alisema Kamanda Issah
Vile vile amesema watuhumiwa waliweza kuonyesha vifaa vilivyotumika katika kutekeleza mauaji hayo ikiwe Nyundo na Sululu huku sehemu za miili ya marehemu ikiwemo kichwani zikiwa zimeharibiwa kikatili.
Ametoa rai kwa jamii ya mkoa wa Njombe kuacha imani za kishirikina zinazopelekea mauaji ya kutisha kwa kuwa asilimia kubwa ya watuhumiwa walioko katika magereza ya mkoa huo yametokana na kesi za mauaji huku wengi wao wakiwa ndugu waliotekeleza kutokana na migogoro ya aina mbali mbali.