Yanga: Tunapindua Meza, Tulieni





UONGOZI wa Klabu ya Yanga kwa kushirikiana na benchi la ufundi la timu hiyo, umeandaa mikakati mizito ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ili washiriki michuano ya kimataifa kwa nguvu zao wenyewe na siyo kubebwa.

 

Ipo hivi, Tanzania itatoa timu nne katika ushiriki wa michuano ya kimataifa baada ya kufanikiwa kufuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Yanga huenda itakuwa kati ya timu hizo zitakazoshiriki michuano ya kimataifa hata kama ikikosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara unaotetewa na watani wao, Simba katika msimu huu.

 

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema kuwa timu yao itakwenda kucheza kimataifa kwa nguvu zao wenyewe na siyo kubebwa na timu yoyote.



Bumbuli alisema kuwa wamepanga kurejea upya katika ligi mara itakapoanza kwa kuhakikisha wanapambana ndani na nje ya uwanja ili kuhakikisha wanabeba makombe yote wanayoshiriki ambayo ni ya ligi na FA kwa lengo la kushiriki michuano ya kimataifa.

 

Aliongeza kuwa hakuna kitakachoshindikana kwao katika hilo huku akiwataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza uwanjani katika kila mchezo kwa kuanzia dhidi ya KMC utakaopigwa kesho Jumamosi saa moja kamili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.“

 

Malengo yetu yapo vilevile katika msimu huu ni kutwaa ubingwa wa ligi kuu ili tushiriki michuano ya kimataifa baada ya kutoshiriki kwa kipindi cha miaka mitatu.

 

“Niwaondoe presha Wanayanga kwa kuwaambia kuwa, tutakwenda kushiriki kimataifa kwa nguvu zetu wenyewe bila kuitegemea timu yoyote na hiyo ndiyo sababu ya kubadilisha benchi la ufundi kwa haraka,” alisema Bumbuli.

 

Katika hatua nyingine, gazeti hili limepata taarifa za kuwarejesha baadhi ya mabosi waliokuwemo kwenye Kamati ya Ufundi na Mashindano ya timu hiyo, iliyokuwa inaoongozwa na Samwel Luckumay, Said Ntimizi na Hussein Nyika.

 

Mabosi hao ndiyo walioiwezesha Yanga kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi katika msimu uliopita wakati wakiwa na kikosi kibovu chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu Mkongomani Mwinyi Zahera.

 

Mabosi hao juzi Jumatatu walikuwa ni sehemu ya viongozi waliofika kuutazama mchezo wa kirafiki Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam uliomalizika kwa Yanga kuwafunga African Lyon mabao 3-0.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad