MSHAMBULIAJIwa zamani wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe amesema uongozi wa klabu hiyo umemlipa fedha alizokuwa anawadai lakini amesisitiza hana uhakika na hilo hadi atakaporejea nchini Burundi kuangalia kwenye akaunti yake.
Tambwe ametoa kauli hiyo baada ya Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Yanga, Hassan Bumbuli kusema kuwa tayari wameshamalizana na mchezaji huyo kwa kulipa dola 22,791 sawa na Sh 52,603,000 kama walivyoelekezwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Akizungumza na Championi Ijumaa, Tambwe alisema kuwa amepigiwa simu na viongozi wa Yanga ambao wamemueleza kuwa wameshamlipa fedha zake kwa kuziweka kwenye akaunti yake kama walivyoelekezwa na FIFA, hivyo amesisitiza atajua ukweli atakapokuwa amerejea kwao Burundi.
“Unajua kwa sasa nipo Djibouti namalizia mechi moja ya ligi na nimefunga mabao 17 katika mechi 16 lakini kuhusu Yanga ni kweli walinipigia simu viongozi na kuniambia kwamba tayari wameshalipa fedha ambazo nilikuwa nawadai kipindi cha nyuma kwa kuweka kwenye akaunti yangu.
“Nimewakubalia ila bado sina uhakika kwa sababu kwa sasa nipo mbali na nchi yangu, hivyo ni vigumu kujua kama kweli wameweka ila kwa kuwa ligi namaliza hapa ndani ya siku tatu nitakuwa Burundi ndiyo nitaamini kama kweli wameniwekea kama walivyosema wenyewe,” alisema Tambwe.
STORI: IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam