Mamlaka ya kitaifa ya magereza nchini Nigeria imethibitisha kwamba zaidi ya wafungwa 1,800 wametoroka jela nchini humo kufuatia shambulio la watu waliojihami kwa bunduki, maafisa walisema.
Washambuliaji hao waliripotiwa kuvamia gereza hilo lilipo katika mji wa kusini mashariki wa Owerri kwa kutumia vilipuzi.
Wafungwa sita wameripotiwa kurejea huku wengine 35 wakikataa kutoroka..
Polisi wanalaumu shambulio hilo lilifanywa na kundi linalotaka kujitenga la wenyeji wa Biafra, ambalo lilipigwa marufuku. Kundi hili limeripotiwa kupinga madai hayo..
Mamlaka ya usimamizi wa magereza imethibitisha ni wafungwa 1,844 waliotoroka gerezani katika jimbo la Imo.
Watu waliokuwa wamejihami wa silaha nzito nzito walivamia kituo cha kuwazuilia wafungwa mjini Owerri mapema Jumatatu, baada ya kuwasili wakiwa wamepanda gari aina ua pick up na mabasi, maafisa walisema.
Msemaji wa polisi alisema washambuliaji hao walitumia maroketi, maguruneti na silaha nyingine katika uvamizi huo.
Rais Muhammadu Buhari ametaja shambulio hilo kuwa "kitendo cha ugaidi". Ameelekeza vikosi vya usalama kuwakamata washambuliaji hao pamoja na wafungwa waliotoroka.
Msemaji wa vuguvugu la watu Biafra wanaotaka kujitenga aliliambia shirika la habari la AFP kwamba madai kuwa lilihusika na shambulio la Jumatatu ni "uongo".
Jimbo la Imo kwa muda mrefu limekuwa eneo linalokuza makundi ya watu wanaotaka kujitenga ,huku uhusiano kati ya serikali kuu na wenyeji wa jamii ya Igbo ukiwa wa mvutano.
Tangu mwezi Januari vituo kadhaa vya polisi na magari katika eneo la kusini mashariki mwa Nigeria yameshambuliwa na silaha kuibiwa. Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na mashambulio hayo.