Zitto: Rais Samia kaanza vizuri lakini tusibweteke







Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoapishwa kushika madaraka baada ya kifo cha hayati John Magufuli, wananchi wamekuwa na matumaini makubwa na utawala wake, lakini ameonya hawapaswi kubweteka na utawala huo.


Rais Samia aliapishwa Machi 19 baada ya kifo cha Rais Magufuli, aliyefariki Machi 17 jijini Dar es Salaam.



Akizungumza juzi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisi za Mwananchi zilizoko Tabata Relini jijini Dar es Salaam, Zitto alisema Rais Samia ana jukumu kubwa la kulinda imani anayopewa na wananchi kwa kufanya mabadiliko ya kisheria ya mifumo iliyopo sasa.



“Nyinyi pia ni mashahidi, tangu tumempata Rais Samia kumekuwa na matumaini makubwa ya wananchi. Mimi nimetoka nje ya Dar es Salaam, juzi nilikuwa Mwanza, jana nilikuwa Kibondo (Kigoma), unaona kuna mabadiliko makubwa. Matumaini ni makubwa.



“Naamini kabisa Mama Samia hatawaangusha Watanzania. Bali mabadiliko haya haya yatakuwa ya kiuchumi na mabadiliko ya kutenda haki. Kama mlivyosikia amesema hataki dhulma, ina maana katika maisha yake yote anasema hataki dhulma,” alisema Zitto.



Huku akitoa mfano wa wafanyabiashara wa fedha za kigeni jijini Arusha waliotakiwa kusalimisha fedha zao Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Zitto alisema Rais Samia amewatoa Watanzania kwenye enzi za kudhulumiwa na kunyimwa uhuru wa maoni.



“Inatia matumaini makubwa ya kuondokana na miaka ya watu kudhulumiwa bila kusema chochote. Yaani tulifikia wakati katika nchi hii, unapigwa halafu unazuiwa usilie. Ukilia unaulizwa kwa nini unalia?” alisema.



Alisema kwa jumla Rais Samia amependezesha makundi yote ya Watanzania, wakiwamo wananchi waliokuwa wakilalamikia ukata wa fedha.



“Alipokuwa akihutubia alisema watu wanalalamika kwamba hawana fedha mifukoni, kwa hiyo anakwenda kujibu kilio cha wananchi hao,” alisema.



Akifafanua zaidi kuhusu matumaini yake, Zitto alisema katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Muhambwe mkoani Kigoma chama chake hakijapata misukosuko waliyoizoea.



“Zamani kuchukua fomu tu ya kugombea, utakuta msimamizi amefunga ofisi, lakini tumekwenda msimamizi wa uchaguzi anamsubiri mgombea.



“Tumewekewa pingamizi na CCM, katika hali ya kawaida tulikuwa tunajua tumeshaenguliwa. Hivi CCM wanaweza kuweka pingamizi bila kuwa wameshaongea na mkurugenzi kabla? Tukajibu kwa taratibu zinazotakiwa, halafu mkurugenzi akatupilia mbali pingamizi la CCM.



“Ni kitu ambacho unajiuliza kama kweli yanatokea? Kwa hiyo ni matumaini makubwa sana. Lakini haya matumaini yasituondoe kwenye mstari kwamba mabadiliko haya yanahitaji mabadiliko ya kimfumo,” alisema.



Aidha, Zitto alisema ni jambo la kujivunia kwa Watanzania kuweza kubadilishana madaraka kwa amani.



“Tukumbuke nchini Malawi baada ya aliyekuwa Rais, Bingu wa Mutharika kufariki ilikuwa ni kashkash kubwa, ilibidi mkuu wa majeshi apeleke vifaru nyumbani kwa aliyekuwa makamu wa Rais kumlinda ili aweze kuchukua urais kwa mujibu wa Katiba. Hatukuyaona hayo Tanzania,” alisema Zitto huku akilipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).





Aonya wananchi kubweteka na matumaini



Kwa upande mwingine, Zitto aliwataka Watanzania kutobweteka na utawala wa Rais Samia, kwani bado hajafanya mabadiliko ya kisheria.



“Tusibweteke, kwa sababu ni mapema mno. Huu ni mwanzo tu, hatujaona shughuli yoyote inayohusisha sheria,” alisema Zitto.



Huku akisisitiza kuwapo kwa mabadiliko ya kimfumo, Zitto alitoa mfano wa kauli ya Rais Samia kuhusu kufunguliwa kwa vyombo vya habari na namna ilivyochukuliwa na watendaji wa Serikali.



“Juzi tumesikia Rais akisema vyombo vya habari vifunguliwe, Katibu Mkuu wa Wizara akasema ni online (mitandao) peke yake, Mkurugenzi wa Habari Maelezo mpya naye akasema ni ‘online’ peke yake, Waziri akaja akasema wenye magazeti waende ofisini kwake wakajadiliane.



“Kwa hiyo yote haya yanaonyesha kuwa tunahitaji mfumo wa kisheria kwa sababu yanaweza kubadilika,” alisema.



Alipoulizwa kama kuna mikakati wanayoifanya ili kuleta mabadiliko ya kisheria na kimfumo, Zitto alisema bado ni mapema.



“Kwanza kuchukuliwa na upepo ni jambo la kawaida, limekuwa likitokea kwenye tawala zote. Kuna watu walikuwa wakosoaji wakubwa wa hayati Magufuli, lakini ndio wamekuwa washangiliaji wakubwa wa Rais Samia,’’ alisema Zitto.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad