Ajibu Anyimwa Mkataba Azam




IMEELEZWA kuwa Azam FC imeweka kando mipango ya kumsajili ya kiungo mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu katika usajili wa msimu ujao kutokana na kutokuwepo katika mipango yao.

 

Ajibu ni kati ya wachezaji ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu wengine ni Miraji Athumani ‘Sheva’, Francis Kahata na Gadiel Michael.

Kiungo huyo alijiunga na Simba katika msimu uliopita akitokea Yanga baada ya mkataba wake wa miaka miwili kumalizika wa kuichezea timu hiyo.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, kiungo huyo hivi karibuni kwa kupitia menejimenti yake iliwafuata mabosi wa Azam FC kwa ajili ya kufanya nao mazungumzo ya kujiunga na kikosi hicho.

 

Mtoa taarifa huyo alisema mazungumzo hayo yalishindwa kufikia muafaka mzuri kutokana na kiungo huyo kutokuwa na vigezo ikiwemo kutokuwepo katika kikosi cha kwanza cha timu yake anayoichezea sasa.

 

“Ngumu kwa Azam kumsajili Ajibu, licha ya menejimenti yake kuonekana kuhitaji mchezaji wao ajiunge na Azam.“Sababu kubwa iliyosababisha kutohitajika ni kushindwa kupata nafasi ya kucheza katika timu yake ya Simba.“

 

Azam hivi sasa wana vigezo vyao walivyoviweka na kati ya hivyo ni lazima kila mchezaji atakayesajiliwa apate nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na siyo kuanzia benchi kama ilivyokuwa kwa Ajibu akiwa na Simba, kibaya zaidi yeye mwenye anataka dau la Sh milioni 100 ambalo ni kubwa aliendani na thamani yake,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa meneja wa kiungo huyo, Hanii Kessy alisema: “Kiukweli hadi hivi sasa hakuna mazungumzo yoyote yaliyokuwepo kati ya Ajibu na timu anayoichezea, kikubwa tusubirie mara baada ya mkataba wake kumalizika itajulikana anakwenda wapi.

 

“Hayo mengine ya kuelezwa kuwa amefanya mazungumzo na Azam ni masuala ya kimtandao pekee ambayo siku hizi mbili yalionekana kuzagaa,” alisema Kessy.

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad