Akanusha Mashitaka ya Mauaji ya Kimbari ‘Nilikuwa Mjamzito’



Mwanamke aliyefukuzwa Marekani na kurejeshwa nchini mwao Rwanda, amekanusha mashitaka ya makosa ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 akisema alipata ujauzito muda mfupi baada ya kujifungua mapacha.“Kuwa na mapacha na kuwa mjamzito, ningewezaje kushiriki kwenye mauaji ninayodaiwa kutekeleza?” ameiambia mahakama.

Béatrice Munyenyezi anakabiliwa na mashitaka saba ya mauaji – yenye kuhusishwa na uhalifu kuanzia mauaji hadi ubakaji.

Kulingana na ushahidi uliotolewa wakati wa kusikiliza kwa kesi ya mume wake na mama mkwe wake katika mahakama ya Umoja wa Mataifa, Arusha, Tanzania, Bi. Munyenyezi alishutumiwa kwa kusimama katika vituo vya ukaguzi barabarani kubaini raia wa Kitutsi ili wauawe na kuhamasisha wanamgabo wa Kihutu kubaka wanawake kabla ya kuwaua huko Butare, mji wa kusini mwa Rwanda.

Akishtumiwa kwa kuwa mwenye ushawishi katika mauaji ya wanafunzi wa Kitutsi mjini humo, Bi. Munyenyezi amekanusha madai hayo akisema alikuwa mgeni na hakuwa ameenda kwenye vituo vya ukaguzi barabarani.

Anasema aliwasili Butare Julai 1993 na kuolewa akiwa na ujauzito wa miezi miwili, akajifungua mapacha na muda mfupi baada ya hapo akapata tena ujauzito mwingine.

Wakati wa kusikilizwa kwa ombi la kuachiwa kwa dhamana Jumatano, akiwakilishwa na mawakili wawili maarufu nchini Rwanda, alikanusha madai yote.

Pia alishutumu baadhi ya mashahidi katika mahakama ya Arusha kwa kusema uongo kuwa walisoma naye Chuo Cha Taifa cha Rwanda kabla ya kutokea kwa mauaji ya kimbari wakati yeye “alikuwa hata hajamaliza shule ya sekondari”.

Mwaka 2011, Arsène Shalom Ntahobali – Mume wa Munyenyezi – na mama mkwe wake Pauline Nyiramasuhuko, aliyekuwa waziri wa masuala ya wanawake, walikuwa mwanamke wa kwanza na kijana wake kupatikana na hatia ya mauaji yaliyotekelezwa Butare wakati wa vita vya kimbari mwaka 1994.

Wawili hao wanahudumia kifungo cha miaka 47 nchini Senegal. Mahakama itatoa uamuzi wake Jumatatu juu ya ombi la kuachiwa kwa dhamana lililowasilishwa na Bi. Munyenyezi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad