Amaliza Utata Bao la Yacouba





WAKATI Yanga jana ikilazimishwa suluhu na Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, gumzo kubwa ni kukataliwa kwa bao la Yanga lililofungwa na Yacouba Songne dakika ya 73 kwa kona iliyochongwa na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’.


Yacouba ambaye aliukwamisha mpira huo kimiani kwa kichwa akiunganishwa pasi ya kichwa kutoka kwa Tuisila Kisinda, lakini bao hilo lilikataliwa kwa tafsiri kwamba mpira ulitoka nje kabla ya mfungaji hajafunga bao hilo.


Kukataliwa kwa bao hilo, kukawafanya wachezaji wa Yanga, kumzonga mwamuzi wa pembeni ambaye aliokolewa na mwamuzi wa kati, Hans Mabena.


Mwamuzi mstaafu aliyekuwa akichezesha mechi za Ligi Kuu Bara, Othman Kazi, amemaliza utata huo kwa kuliambia Spoti Xtra kwamba: “Kabla ya mpira kumfikia Yacouba, mpira ulikuwa umetoka nje na kurudi uwanjani, hivyo haliwezi kuwa bao halali ndiyo maana mwamuzi wa pembeni alinyoosha kibendera juu kabla hata bao halijafungwa kuashiria kwamba kuna makosa yamefanyika.



”HALI YA MCHEZO

Katika mchezo huo, licha ya jitihada za nyota watatu walioanza kikosi cha kwanza ndani ya Yanga ambao ni Kisinda, Michael Sarpong na Saido, hakuna ambaye aliona lango la mpinzani wake.


Namungo wataijutia nafasi ya wazi ambayo waliikosa kupitia kwa Hashim Manyanya dakika ya 8 ambaye alikuwa ndani ya 18, akapiga shuti lililokwenda nje kidogo ya lango la Yanga, huku Yacouba naye ataikumbuka nafasi aliyokosa dakika ya 66 baada ya kipa Jonathan Nahimana kuokoa hatari.Saido alipiga jumla ya pasi 22, alikokota mpira mara tano huku akipiga jumla ya faulo tatu na kona 7.


Sarpong alitumia jumla ya dakika 62 na nafasi yake ilichukuliwa na Ditram Nchimbi ambapo alipiga jumla ya pasi 21, mashuti yaliyolenga lango yalikuwa mawili na mawili hayakulenga, huku akichezewa faulo nne.



Kisinda spidi zake zilikuwa zikipambana na Jafary Mohamed, alipiga pasi 33, alikuwa kwenye ubora wake licha ya Uwanja wa Majaliwa kuwa na changamoto kutokana na ubora kuwa mdogo sehemu ya kuchezea.

 

Suluhu hiyo imezidi kufifisha matumaini ya Yanga kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo sasa imefikisha pointi 58 ikiwa pointi tatu nyuma ya vinara Simba wenye 61.Yanga mpaka sasa imecheza mechi 28, imebakiwa na mechi sita kukamilisha msimu huu, huku Simba ikicheza mechi 25, ina mechi tisa mkononi kihitimisha msimu.

 

Katika mechi tisa ilizobaki nazo Simba, inahitaji ushindi wa mechi tano tu ili kutangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo itakuwa imefikisha pointi 76. Kumbuka katika mechi hizo, miongoni mwayo itakuwa ni ile dhidi ya Yanga.Yanga ikiwa imebakiwa na mechi sita, ikishinda zote itamaliza msimu na pointi 76.

STORI: BRAHIM MUSSA, LINDI


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad