ANGELINA George ndiyo majina yake halisi ila kwa wapenzi wa muziki wake kunako Bongo Flevani, wanamnyaka kwa jina la Anjella TZ.
Ni pisi moja matata utoka Tanga moja; kule mahaba yalipozaliwa. Wenyewe huwa wanasema mchele unalimwa Mbeya, lakini wali unapikwa Tanga.Anjella ni first lady wa Lebo ya Konde Gang Music Worldwide (KGMW).
Kwa sasa anakiwasha na ngoma yake inayokwenda kwa jina la Kama.Kabla ya hapo, Angella alisikika kwenye Ngoma ya All Night.
Kama kawaida yake ya kutoa fursa kwa vipaji vipya kukua, IJUMAA SHOWBIZ imekaa kitako na Angella kwenye exclusive interview ambaye anafunguka mambo kibwena juu ya milima na mabonde aliyopitia kwenye safari yake ya muziki ikiwemo kunyanyasikia, kudhalilika na kutengwa na baadhi ya watu kumtokana na hali yake aliyonayo;
IJUMAA SHOWBIZ: Hongera kwa kuwa msichana wa kwanza kusajiliwa Konde Gang…
ANJELLA: Kwanza nashukuru Mungu, mimi ni msichana ambaye nimeamua kupambana hadi nimefikia hapa na sikutaka kukata tamaa.IJUMAA SHOWBIZ: Mashabiki wangependa kufahamu msoto uliopitia hadi kufikia hapa ulipo…
ANJELLA: Kwanza nimefurahi sana kupata nafasi ya kufanya mahojiano na Gazeti la IJUMAA kwa sababu ni fursa kubwa mno.
Pia kwenye maisha yangu nimepita kwenye mambo mengi. Nimedharaulika sana, nimenyanysika sana. Ni vitu ambavyo hata nikikaa na kuwaza vinaniumiza sana, ila nashukuru kwa kutokukata tamaa kwangu, ndiyo kumenifanya hadi leo nikawa hapa nilipo.
Nakumbuka niliwahi kwenda studio moja kwa ajili ya kurekodi wimbo f’lani, lakini kwenye video akawekwa mtu mwingine wakati wimbo ulikuwa ni wangu. Nilipouliza kwa nini nimefanyiwa hivyo, nikaambiwa umefanyiwa hivi kwa sababu ya hali yako (tatizo la kuvimba miguu) huwezi kuwa kwenye video. Kiukweli ni jambo ambalo lilikuwa linaniumiza sana.
IJUMAA SHOWBIZ: Watu wengi hawajui umetokea wapi; yaani historia yake kwa ufupi?
ANJELLA: Mimi ni mzaliwa wa Tabora, baba yangu ni mnyamwezi ila mama yangu ni mtu wa Tanga na nimekulia huko na kulelewa Dar na mpaka sasa ninaishi Dar.
IJUMAA SHOWBIZ: Ulijisikiaje ulipotangazwa kuwa msanii wa Konde Gang?
ANJELLA: Nilipotangazwa kwamba mimi ni msanii wa Konde Gang rasmi, kiukweli nilishikwa na furaha ya ajabu na nikaanza kufikiria kwamba na mimi nikianza kujitambulisha, nitasema natokea Konde Gang; yaani unajua kuna mambo mengi ambayo niliyawaza sana.
IJUMAA SHOWBIZ: Ushirikiano wako na wasanii wengine wa Konde Gang ukoje?
ANJELA: Upo vizuri sana na ninashukuru sana Mungu kwa amani ipo kubwa. Pia ninajisikia kama nipo nyumbani kiukweli.
IJUMAA SHOWBIZ: Unajisikiaje kufanya kazi na msanii mkubwa kama Harmonize ambaye ndiye bosi wako?
ANJELLA: Kufanya kazi na Harmo kiukweli ni raha zaidi ya raha mpaka najiona kama ni mtu mwenye bahati kubwa, maana ni msanii mkubwa sana. Ni msanii ambaye kila mtu anatamani kufanya naye kazi. Sina cha kumlipa, lakini Mungu ndiye atamlipa.
IJUMAA SHOWBIZ: Harmonize ni mtu wa aina gani kwako?
ANJELA: Ni mtu ambaye naweza kumuita muongoza njia kwa sababu ni mtu ambaye ameweza kunitoa kunako kudharaulika na kutengwa na ameniheshimisha, sasa hivi Anjella ninaheshimika.
IJUMAA SHOWBIZ: Kufanya kazi na Harmonize ni kitu gani ambacho kimeongezeka kwenye maisha yako?
ANJELLA: Kitu ambacho kimeongezeka kikubwa kwangu mimi ni heshima katika familia yangu na hata kwangu pia na watu ambao walikuwa hawapo karibu na mimi, kwa sasa hivi naona kabisa wanakuja na wengine wananipa ushauri.
IJUMAA SHOWBIZ: Ilikuchukua muda gani hadi kuingia rasmi Konde Gang?
ANJELLA: Kusajiliwa Konde Gang ilinichukua wiki chache tu kisha nikatangazwa.IJUMAA SHOWBIZ: Utaratibu ukoje labda, kuna mkataba wowote ambao umesaini?
ANJELLA: Ndiyo nimeshapata mkataba mnono.
IJUMAA SHOWBIZ: Na ni wa muda gani?ANJELA: Ni wa muda mrefu, ila sitaweza kusema ni miaka mingapi mambo mengine ni jukumu la menejimenti.
IJUMAA SHOWBIZ: Kufanya kazi na Harmo inakupa ugumu gani?
ANJELLA: Ugumu upo kwa sababu ni Harmo ni msanii mkubwa na anajua mambo mengi kwenye muziki, halafu mimi bado nina hofu, mtu kukutana na fundi kama Harmo unaona kama utakosolewa sana.
IJUMAA SHOWBIZ: Ngoma ya Kama ni idea yako au kuna mtu nyuma ya pazia ndiye anafanya hayo?
ANJELLA: Ni idea ambayo ilifanyika studio tukiwa na Harmonize na timu nzima ya Konde Gang, tukawa tunajadiliana hadi wimbo ulivyokamilika.
IJUMAA SHOWBIZ: Ulijisikiaje kufanya ngoma ya kwanza na Harmo na ikaingia kwenye trending.ANJELLA: Nilijisikia vizuri kufanya kazi na kuweza kuingia kwenye trending kwa mara ya kwanza, japokuwa kwa Harmo kushika namba moja ni kawaida.IJUMAA SHOWBIZ: Imekupa nguvu kiasi gani?
ANJELLA: Imeweza kunibusti kwa asilimia kubwa na kunionesha njia kwenye muziki wangu. Ninamuombea sana kwa Mungu azidi kumpa njia na riziki kubwa zaidi ya hapo alipo.
IJUMAA SHOWBIZ: Umekuwa ukishindanishwa sana na msanii mwenzako kutoka Lebo ya Wasafi, Zuchu labda kwako inakupa picha gani?
ANJELLA: Unajua mashabiki kila mmoja huwa anakuwa na fikira yake, kwa hiyo huwezi kumzuia mtu kukuongelea au kukushindanisha ni kitu ambacho nimezoea kukiona kwa wasanii walionitangulia na kwangu pia kimenikuta. Kwa hiyo kuna ule uzoefu kwamba nikifika steji f’lani nitakutana nacho.
IJUMAA SHOWBIZ: Vipi kuhusiana na ile kolabo yako na Yemi Alade wa Nigeria ambayo Harmonize amewaahidi mashabiki? Mbona kama hakuna kinachoendelea? Tuitegemee lini?
ANJELLA: Kolabo yangu na Yemi Alade ni menejimenti imepanga itaachiwa lini, lakini kila kitu kipo tayari.
IJUMAA SHOWBIZ: Miezi michache iliyopita, Harmo alisema kuwa atakupeleka nchini India kwa ajili ya matibabu ya miguu yako, vipi suala hilo mpaka sasa linaendeleaje?
ANJELA: Kuhusu mimi kutibiwa ni jambo ambalo kwa sasa hivi ndiyo linafanyika, nipo kwenye matibabu kwa sababu Harmo alisema ikishindikana Tanzania ndiyo nitapelekwa India.
IJUMAA SHOWBIZ: Ni mambo gani ambayo huwa yanakukera zaidi kwenye mitandao ya kijamii?
ANJELLA: Ni watu kunisema vibaya. Mimi sijapenda kuwa hivi. Hii ni mipango ya Mungu tu na pia nina imani nitapona.
IJUMAA SHOWBIZ: Unajiona nani miaka michache baadaye kupitia muziki wako?
ANJELA: Najiona Anjella wa tofauti na wa kimataifa, nitakuwa siyo Angella yule ambaye nimetokea kwenye kuimba ‘covers’ za wasanii wenzangu, nitakuwa mtu wa kolabo za kimataifa kwa sana.
MAKALA: KHADIJA BAKARI