BAADA ya wapinzani wa Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika kutua ardhi ya Bongo wameanza kuwa na wasiwasi juu ya mchezo wao wa kesho unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.
Kaizer Chiefs inayonolwa na Kocha Mkuu, Gavin Hunt ina kibarua cha kulinda ushindi wao wa mabao 4-0 ambao waliupata nchini Afrika Kusini kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa FNB.
Wakati wao wakiwa na hesabu hizo za kulinda ushindi, Simba chini ya Kocha Mkuu, Didier Gomes hesabu zao ni kupindua meza kibabe ili waweze kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali.
Hofu ya kwanza ambayo walikuwa nayo Kaizer Chiefs ni suala la Corona ambapo Mkurugenzi wa Masoko wa timu hiyo, Jessica Motaung amesema kuwa wana wasiwasi juu ya vipimo vya Corona huku akibainisha kwamba wao wapo vizuri.
"Nina wasiwasi juu ya mapokezi ambayo tutayapata Dar. Uzuri ni kwamba tayari wachezaji wetu wote wapo vizuri na hawana Virusi vya Corona,".
Wachezaji ambao walitua jana walikuwa wakilalamikia kwamba wanaamini mchezo utakuwa mgumu ila hawana imani na suala la waamuzi pamoja na hali ya hewa kuwa tofauti kidogo.
Ili Simba iweze kusonga mbele hatua ya nusu fainali inahitaji ushindi wa mabao 5-0 jambo ambalo Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa linawezekana ikiwa wachezaji wataamua.