Kampuni ya Microsoft ilikuwa inamchunguza mwanzilishi mwenza wake, bilionea Bill Gates juu ya madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mfanyakazi wake kipindi kifupi tu kabla ya bilionea huyo kujiuzulu kutoka kwenye bodi ya kampui hiyo mwaka jana.
Kampuni hiyo kubwa ya teknolojia imethibitisha kuwa kuanzisha uchunguzi baada ya kuwasilishwa kwa malalamiko juu ya tabia zake zenye kuzua wasiwasi.
Kampuni hiyo imesema imeshirikiana katika uchunguzi huo na kampuni moja ya sheria na pia ilimsaidia mfanyakazi aliyewasilisha malalamiko yake.
Msemaji wa Bwana Gates amekanusha madai kuwa uamuzi wake wa kujiuzulu ulikuwa na uhusiano wowote na uchunguzi huo.
Taarifa za uchunguzi huo zimeibuka baada ya Bill na Melinda kutangaza uamuzi wao wa kutalikiana baada ya ndoa yao iliyodumu kwa miaka 27.
Jumatatu, msemaji wa kampuni ya Microsoft alisema kuwa kitengo cha kampuni hiyo kilipokea malalamiko mwishoni mwa mwaka 2019 kwamba Bwana Gates “alitaka kuwa na uhusiano wa kimapenzi” na mfanyakazi wa kike mwaka 2000.
“Kamati ya bodi ilishughulikia jambo hilo kwa usaidizi wa kampuni moja ya sheria kutoka nje kufanya uchunguzi wa kina,” alisema.
Bill na Melinda Gates
“Wakati wote wa uchunguzi huo, kampuni ya Microsoft ilitoa ushirikiano wake stahiki kwa mfanyakazi aliyewasilisha malalamiko,” aliongeza.
Uchunguzi huo haukufikia tamati, kwa sababu Bwana Gates alijiuzulu katika bodi hiyo kabla ya uchunguzi kukamilika.
Katika ujumbe katika mtandao wa LinkedIn Machi mwaka jana, Bwana Gates alisema alichukua uamuzi huo ili aweze kuwa na muda wa kutosha kufanya kazi na taasisi yake ya kusaidia watu ya Wakfu wa Bill na Melinda Gates. Pia uamuzi huo ulitokea miezi mitatu baada ya kuchaguliwa tena kuhudumu kwenye bodi hiyo.
Wakati huo, aliandika: “Kwa heshima ya kampuni ya Micrososft, kujiuzulu kwenye bodi hakumaanishi kujiondoa kwenye kampuni. Microsoft itaendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha yangu… Najihisi mwenye matumaini zaidi kuhusu maendeleo yanayopigwa na kampuni hii na vile inavyoweza kuendelea kufaidisha dunia.”
Hata hivyo, gazeti la Wall Street Journal la Jumapili lilisema kuwa bodi ya kampuni ya Microsoft ilifikia uamuzi kwamba hatua ya Bwana Gates kujihusisha na mfanyakazi wa kike kimapenzi haikuwa sawa na alihitajika kujiuzulu.
Msemaji wa Bwana Gates alikiri kuwa uhusiano huo ulikuwepo baada ya kuulizwa na gazeti hilo, lakini alikanusha kwamba ulikuwa na uhusiano wowote na uamuzi wa kujiuzulu.
“Uhusiano huo ulikuwepo karibu miaka 20 iliyopita ambao pia uliisha kwa njia ya amani,” msemaji huo alisema.
“Uamuzi wa Bill wa kujiondoa kwenye bodi haukuwa na uhusiano wowote na suala hili. Ukweli ni kwamba, alikuwa ameonesha nia yake ya kujiuzulu mara kadhaa akitaka kuwa na muda zaidi na wakfu wake miaka kadhaa kabla.”
Wakfu wa Bill na Melinda Gates uliiambia BBC kuwa unasimama na taarifa ya msemaji wa Gates.
Bill na Melinda Gates walitangaza uamuzi wao wa kutalakiana mapema mwezi huu. Wawili hao wametumia mabilioni ya pesa katika shughuli za kusaidia watu kote duniani na wameahidi kuendelea kushirikiana katika shirika lao baada ya mchakato wa talaka yao kukamilik
Vyombo vya habari vya Marekani viliripoti kuwa wawili hao walikubaliana kugawana mali zao kabla ya kutangaza kwamba watatengana.
Bwana Gates, 65, ni wa nne kwa utajiri duniani, kulingana na jarida la Forbeds, ambaye thamani yake ni dola bilioni 124 (£89bn).