MBUNGE wa Viti Maalum Ester Amos Bulaya ameitaka Wizara ya Maji kuziba mianya ya upotevu wa maji ili kuokoa pesa za serikali zinapotea katika miradi ya maji iliyopo nchini ilihali bado upatikanaji wa maji bado ni tatizo nchini.
Bulaya amesema hayo katika kipindi cha majadiliano leo bungeni, kuhusu Wizara ya Maji ambapo amesema kama ilivyo kauli ya Waziri wa Maji, anayopenda kuitumia inayosema mtu akichezea miradi maji atamzingua, basi ndivyo wabunge watakavyomzingua endapo maji hayatatoka katika majimbo yao.
“Zibeni mianya ya upotevu wa maji kwani pesa zinapotea, wewe unasema wakikuzingua utawazingua na sisi wabunge humu ukituzingua, maji hayatoki katika maeneo yetu na sisi tutakuzingua kabla ya Rais hajakuzingua,” amesema Bulaya.
wali akichangia hoja kuhusu Wizara ya Maji ameeleza kukinzana kwa tathimini kati ya zinazotelewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kulingana na upatikanaji wa maji nchini.
“Tujiulize hizi tathimini tunazopewa, EWURA inasema Mkuranga, Kisarawe na Chalinze upatikanaji maji ni asilimia 99, ripoti ya CAG amesema ni asilimia 53 kwa hiyo takwimu tunazopewa na Wizara na upotevu wa maji inawezekana upatikanaji wa maji nchini haufiki hata asilimia 50,” amesema Bulaya.
Wakati huo huo Mbunge wa Dodoma Mjini Antony Mavunde ameiomba Wizara ya Maji kuangalia upya matumizi ya ‘force account’ katika miradi ya maji kwani imekwamisha upatikanaji wa maji kwa watanzania.