DC Sabaya aingilia kati maiti kuzuiwa mochwari wilayani Hai




Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya ameagiza ndugu kuchukua mwili wa,  Bauda Nkya (68) aliyefariki dunia siku saba zilizopita katika hospitali ya KCMC  lakini ulizuiwa kutokana na deni  la Sh3.5 milioni.


Amesema kiasi hicho cha fedha kitatolewa na ofisi yake ili mazishi ya Nkya aliyekuwa mkazi wa kijiji cha Nshara kata ya Machame Kaskazini yafanyike.



Mwanamke huyo alifariki dunia Mei 2, 2021 baada ya kujikwaa kwenye kisiki na kupata jeraha mguuni.



Akizungumza mara baada ya kuitembelea familia ya marehemu Sabaya amesema, “nilishawahi kusema na Waziri naye alishasema kwamba haya mazingira ya mtu akishakufa kibinadamu ni mazingira ya taabu na dhiki kinachotakiwa kufanyika ni kusaidiana ili maisha mengine yaendelee.”



"Kwa kweli maisha ya hapa kwenye hii familia ni duni na walikuwa wakisaidiwa na Tasaf..., kwamba ii familia ilipe hizi gharama ni miujiza kabisa. Poleni sana kwa msiba  huu wa mama yetu ,Serikali inatambua kilio chenu ofisi yangu kupitia kwa katibu tawala atafanya mawasiliano na mwenyekiti wa kijiji hiki ili mwili uletwe kesho kwa ajili ya maziko.”



Sabaya aliitaka familia hiyo kuendelea na maandalizi ya mazishi na kwamba ofisi yake itasimamia.



Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa Hospitali hiyo, Gileard Masenga amesema taarifa hizo hana na kwamba upo utaratibu  endapo mtu ameshindwa kulipa gharama.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad