TANGU Jumatatu, Wapiganaji wa Hamas wamerusha makombora 1000 katika ardhi ya Israel mengi yakilenga mji mkuu wa Tel Aviv na maeneo yake nao wanajeshi wa Israel wakifanya mashambulizi ya mabomu katika ukanda wa Gaza na kuwauwa makumi ya raia.
Lakini Israel ina kinga yenye uwezo mkubwa kujilinda dhidi roketi zinazorushwa na Hamas kutoka Gaza , kwa jina ‘Iron Dome’.
Kama ilivyoripotiwa na jeshi la Israel, kati ya roketi 1050 zilizorushwa, 850 zilitunguliwa na mfumo huo wa kutungua makombora.
Mfumo huu ni mojawapo ya mifumo ya kulinda anga ya Israel,lengo lake kuu ni kulinda taifa hilo dhidi ya silaha za masafa marefu, roketi na vitisho vingine.
Jinsi mfumo wa Iron Dome unavyofanya kazi
Mfumo huo uliundwa na kampuni ya Rafael Advanced Defence System Ltd, kampuni ya kibinafsi inayoshirikiana kwa ukaribu na jeshi la Israel ambayo pia hutengeza mifumo ya kinga ya baharini na majini ya taifa hilo.
Kampuni hiyo pia inafadhiliwa na Marekani kwa takriban US $ 200m, mtengenezaji wake anahakikisha kuwa ni mfumo unaotumiwa sana kutungua makombora angani duniani na kwamba umefanikiwa kufanya kazi katika matukio asilimia 90.
Betri za mfumo huo hutengenezwa kwa kutumia makombora ya kutungua makombora, Rada na mifumo inayochambua ni wapi kombora la adui litaanguka.
Teknolojia ya Rada inatofautisha kati ya makombora ambayo yanaweza kufika katika miji na yale yanayokosa lengo lake. Mfumo huo baadaye unaamua ni kombora gani linafaa kutunguliwa.
Silaha hiyo ya kutungua makombora hurushwa wima kutoka kwa mfumo huo. Baadaye hutungua makombora hayo angani.
Chanzo cha mfumo huo wa Iron Dome ni mzozo wa 2006 nchini Israel dhidi ya kundi la Hezbollah, wapiganaji wa Lebanon.
Hezbollah wakati huo ilirusha maelfu ya roketi , na kuwaua makumi ya Waisraeli na kusababisha uharibifu mkubwa.
Hatahivyo juhudi za Israel kujenga mfumo wa kinga ya makombora ulianza miongo mitatu iliopita na ni kutokana na ushirikiano kati ya jeshi la Marekani na Israel.
Mwaka 1986, Israel ilitia saini kandarasi na Marekani ili kufanya utafiti kuhusu mfumo wa kujilinda dhidi ya makombora ya masafa marefu, mradi ulioanzishwa na utawala wa rais Ronald Reagan wa Marekani.
Miaka mitano baada ya makubaliano hayo , viongozi wa Israel walisukuma juhudi za kujenga mfumo huo wakati rais wa Iraq Saddam Hussein alipoagiza kurushwa kombora la Scud nchini Israel wakat wa vita vya kwanza vya Ghuba.
Kufikia mwanzo wa 2010, silaha ya Iron Dome ilikuwa imefanikiwa kupita majaribio yaliofanywa na jeshi la Israel.
Chanzo BBC.