Gwajima: Ni Ujinga Kuruhusu Taifa Kuwa Majaribio Chanjo ya Corona




Mbunge wa Kawe (CCM), Askofu Josephat Gwajima ameshauri Serikali kuwa makini na madhara yanayoweza kujitokeza kwa wananchi iwapo Taifa litaruhusu chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona kutumika nchini.

 

Gwajima ameyasema hayo leo Jumanne Mei 11, 2021 wakati akichangiwa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mwaka 2021/22. Amesema hayuko kinyume na chanjo bali yuko makini na aina ya chanjo za ugonjwa huo.

 

Huku akitaja aina tatu za chanjo ya ugonjwa huo, amebainisha kuwa ni tofauti na chanjo nyingine zilizokuja duniani ambazo zilikuwa zikichukua kati ya miaka nane hadi 10 kabla ya kuanza kutumiwa.

 

“Mtu asininukuu kwamba ninapinga chanjo hapana, mpaka sasa tunazo chanjo nyingi zinaendelea ikiwemo polio, kifaduro, surua, homa ya ini na nyingine nyingi. Dunia imekuwa na chanjo aina ya attenuation ambapo virus wanapunguzwa nguvu wanaingizwa mwilini halafu antibodies zina react na kutengeneza kinga.

 

“Kinga hii inachukua miaka nane mpaka 10 kukamilika kutengenezwa, lakini chanjo ya corona ni chanjo ya mwendo kasi, miezi miwili minne imekamilika, unapojaribu kuuliza kwa nini inakuwa haraka wanasema sababu ni kukuwa kwa teknolojia, wamemobilize resources na pandemic.

 

Amesema aina hiyo ya chanjo haijajulikana kuwa atazaliwa mtu wa namna gani baada ya miaka 10, kwamba kwa kawaida chanjo zote kabla ya kutumika ni lazima ziwe zimeruhusiwa na taasisi za nchini Marekani za CDC na FDA.

 

“Tofauti ya utu wa mtu na mnyama ni DNA, RNA na genes, chanjo hii inaingia kwenye DNA, RNA na genes, hatujajua chanjo hii atazaliwa mtu wa namna gani baada ya miaka mitano, sita ama 10 ijayo.

 

Hata hivyo, amesema chanjo ya corona hazikuruhusiwa na taasisi hizo bali zimeruhusiwa na mamlaka ya dharura ambayo inasema madhara yanayotokana na chanjo hiyo ni juu ya mtumiaji mwenyewe.

 

“Kwenye website ya chanjo ya JohnsonJohnson wameandika madhara ya chanjo hii ni kushindwa kupumua sawasawa, kuvimba kwenye uso, mapigo ya moyo, damu kuganda…. AstraZeneca wao wameandika inasababisha kuganda damu na kifo.

 

“Tukikataa chanjo tunaweza kuzuiwa kwenda Ulaya, sasa tunakabiliwa na uchaguzi mbaya sana, tuchanjwe kitu tusichokijua sawasawa, au tusichanjwe tuziwe kwenda Ulaya.

 

“Serikali na wizara ya afya wawe makini wanapochagua chanjo hizi waangalie madhara ya sasa, siku zijazo na Taifa. Tatizo tulilonalo ni kudhani kila kinachotoka Ulaya kinatufaa sisi.

 

“Jana kati ya watu waliotengeza chanjo hizi ameandika barua kwa Rais wa Marekani akisema chanjo hizi zisitishwe mara moja kwa sababu madhara yake huko baadaye ni makubwa kuliko sasa,” amesema.

 

“Miaka ijayo tunaweza kuwa na taifa lisilo na watu wanaoweza kufikiri vizuri na kufanya maamuzi sawasawa, ni ujinga kuruhusu taifa zima kuwa majaribio eti kwa sababu tuna haraka ya corona,” amesema Gwajima.

 

Ameitaka wizara ya Afya kabla kuamua kuitumia wawe na wataalam watakaoangalia kwa makini vitu vilivyomo kwenye chanjo hiyo na matatizo watakayoyapata watu watakaozaliwa baadaye. Amesema ni ujinga mkubwa kuruhusu majaribio ya chanjo hiyo kwa Watanzania wote kwa sababu ya haraka.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad