Ameandika Haya Kupitia :
Naomba niandike kuhusu hili la huu utaratibu mpya wa BASATA. Binafsi sikubaliani nalo na ntalipinga kwa nguvu nyingi. Sidhani kama Sheria hii inafaa hata kuwepo achia mbali kutumika. HAINA TIJA YEYOTE,HAIMSAIDII MSANII KWA NAMNA YEYOTE. Ni ya kidwanzi. Inatakiwa kurekebishwa kama sio kuondolewa kabisa. Tutafute namna nyingine za ku’censor sanaa matusi yasisikike kwa kadri inavyowezekana na sio kwa utaratibu huu dhaifu na wa kikandamizaji. Siungi mkono nyimbo “chafu” lakini kutengeneza urasimu usio na msingi kwa kisingizio cha kuwepo kwa nyimbo zisizofaa ni jaribio la kuzorotesha tu sanaa.
Kama BASATA na COSOTA wanataka kutekeleza KILA Sheria inayowahusu wangeanza na Sheria namba 7 ya mwaka 1999 inayowapa Cosota haki ya kutoa leseni kwa maeneo ya hadhara yanayotumia kazi za sanaa,kukusanya MIRABAHA toka maeneo/leseni hizo na kuwalipa wasanii makusanyo hayo.
HIZI NDIO SHERIA ZITAKAZOMSAIDIA MSANII NA WAMEZIFUMBIA MACHO KWA MIAKA MINGI, wasanii wanaendelea kupoteza hela zao NYINGI stahiki na mnawaletea sheria zisizo na kichwa wala miguu kuja kuwakandamiza. BASATA kama mlezi wa wasanii lilitakiwa kusimama kidete mpaka hili la MIRABAHA lifanikiwe.
Bahati nzuri tuna Waziri na Katibu Mkuu wasikivu,tutalisemea kwa namna nyingi hili na tunaamini kero hii itaondolewa haraka.
Msifanye kutoa wimbo iwe kama kuomba passport au VIZA,mnaonea wasanii,tunakwamisha sanaa.
Kwa heshima nyingi nawaambia Basata,mambo ya namna hii ndio haswa yanayotupa kazi kubwa kuwaelezea wapenzi wa kawaida wa sanaa kuwa Baraza hili lina kazi nyingine zaidi ya kufungia na kufungulia tu nyimbo na wasanii.
Na kuweka kumbukumbu sawa, jambo liliwahi kuja kwa majadiliano kwenye Bodi ya Basata wakati nikiwa nahudumu kama MJUMBE wa Bodi,NA NILILIPINGA SANA kwa wakati ule kama nnavyoendelea kulipinga sasa.
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...