MKUU wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amemtaka kamishna Salum Hamdun kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa kiapo chake na kuhakikisha anasimamia sheria na taratibu za nchi ikiwa pamoja na kuwatendea haki wananchi atakaowahudumia.
IGP Sirro amesema hayo wakati akimvalisha Cheo cha Ukamishna wa Polisi CP, Salum Hamdun kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan baada ya Mhe. Rais kumpandisha cheo hicho.
Hata hivyo, IGP Sirro wakati akimvalisha cheo cha Ukamishna pia alimkabidhi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kitabu cha muongozo kinachoongoza Jeshi hilo.
Naye Kamishna mteule CP Salum Hamduni amesema kuwa, ataendelea kutenda kazi zake kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo na kwamba atahakikisha anawatendea haki Watanzania kwa kulinda usalama wao na mali zao.
Kwa upande wake Kamishna wa Kamisheni ya Ushirikishwaji wa Jamii CP Dkt. Mussa Ali Mussa amesema kuwa, Jeshi la Polisi litaendelea kufanya kazi kwa weledi na kwa uaminifu ili kuhakikisha Jeshi linaendelea kujijengea heshima kwa wananchi.
Awali kabla ya kupandishwa cheo hicho na Mhe. Rais, Kamishna Salum Hamdun alikuwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es salaam akiwa na Cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi.