MWANAMAMA anayejua uchungu wa kuzaa ambaye alijipatia umaarufu kupitia Bongo Movies, Jacqueline Wolper Massawe ameibuka na kumtetea vilivyo msanii wa Bongo Fleva, Lulu Eugen ‘Amber Lulu’ akisema ana haki ya kusimama kama mama kwa udhalilishaji aliofanyiwa mtoto wake na msanii wa chipukizi Omary Said ‘Hamorapa’.
Kama Amber Lulu, Wolper ambaye naye amejifungua hivi karibuni, anasema kuwa, amekasirishwa mno na kitendo cha Hamorapa kudai kuwa mtoto wa Amber ni wake na kama angekuwa ni yeye basi angemkata jamaa huyo mkono.
Wolper anasema kwa upande wake asingeweza kuvumilia mpaka udhalilishaji huo.
Hivi karibuni, baada ya Amber Lulu kumuanika mwanaye na mwanaume aliyezaa naye, ghafla Hamorapa aliibuka na kudai kuwa mtoto huyo ni damu yake.
Katika mazungumzo na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, Wolper anasema kuwa, yeye kama mama ambaye amejua taabu ya kujifungua leba, angechukua hatua mbaya dhidi ya Hamorapa kwa sababu kila akikumbuka alivyoteseka, anatamani angekuwa yeye ndiye Amber Lulu kwani angemkata Hamorapa mkono mmoja na akikumbuka tena, angemkata mkono mwingine kwa sababu jamaa huyo hajui uchungu wa kuzaa.
“Yaani huyo Hamorapa aendelee kuwafanyia upumbavu haohao.
“Mimi kwangu angeona cha moto nakuambia, kila nikikumbuka machungu ya leba, ningekuwa ninamkata mkono na nikikumbuka tena, ninakata mkono mwingine au mguu; yaani naumia mno sijui nisemaje.
“Unajua maumivu tunayokutana nayo wanawake ni makubwa mno wakati wa kujifungua, halafu leo mtu anamsema mtoto wangu, aisee sijui nini kingetokea,” anasema Wolper aliyejifungua hivi karibuni.
Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limezungumza na Amber Lulu juu ya sakata lake na Hamorapa ambaye anasema kuwa, chozi alilolitoa kwa sababu ya mtoto wake halitakwenda bure na atahakikisha haki ya kudhalilishwa yeye na mtoto wake inatendeka.
“Mimi mwanzo nilimsamehe, lakini naona kama amejiona mjanja. sasa tutakwenda mbele kwa mbele ndiyo tutajua maana sikubali hata kidogo,” anasema Amber Lulu muda mfupi baada ya kumtia mbaroni Hamorapa, Jumamosi iliyopita katika Hoteli ya Kebbys iliyopo Bamaga jijini Dar, alipokuwa akijiandaa kuzungumza na waandishi wa habari.
Hata hivyo, IJUMAA WIKIENDA lilizungumza na Hamorapa akiwa kwenye gari mara tu baada ya kutiwa mbaroni ambapo aliendelea kusisitiza;
“Hata kama nitauawa mtoto ni wangu, mimi siyo mjinga hata kidogo. Ukweli ni kwamba mtoto ni wangu na yeye (Amber Lulu) anajua hilo.”