Kocha Mkuu wa Kaizer Chiefs, Gavin Hunt ambao ni wapinzani wa Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika amesema kuwa anatambua mchezo wao wa marudio utakuwa na ushindani mkubwa ila wapo tayari kupata ushindi kwenye mchezo huo.
Kaizer Chiefs inatarajiwa kuwasili nchini Tanzania leo Mei 19 ikitokea nchini Afrika kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wao wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.
Hunt amepata umaarufu mkubwa baada ya kuwa kocha wa kwanza kuifunga Simba mabao zaidi ya mawili kwa msimu huu kwenye Ligi ya abingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo wa robo fainali ya kwanza uliochezwa Uwanja wa FNB Soccer City.
Pia picha yake akiwa na furaha baada ya ushindi huo ilizua gumzo kwa mashabiki wengi wa masuala ya soka wakiijadili kwa namna ambavyo walipenda.
Kocha huyo amesema:"Mchezo wa kwanza umekwisha na matokeo yamepatikana, kuelekea mchezo wetu ujao tuna kazi ya kusaka ushindi ili kufikia malengo yetu na tunatambua kwamba haitakuwa kazi rahisi," amesema.