Chama cha Madaktari nchini Tanzania (MAT) kimesema kuwa serikali inapaswa kutoa takwimu sahihi kuhusu maambukizi ya virusi vya Corona kwani takwimu zitairahisishia serikali hata katika utengaji wake wa bajeti katika kujua gharama zitakazotumiaka kupambana na wimbi la ugonjwa huo.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 18, 2021, na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt. Shadrack Mwaibambe, wakati akieleza ni kwa namna gani chama hicho kimeipokea ripoti na mapendekezo yaliyotolewa hapo jana na kamati maalum ya Corona iliyoundwa na Rais Samia Suluhu.
"Suala la takwimu za Corona ni muhimu sana hata katika uchumi kama kuna ugonjwa ambao serikali inahitaji kutumia hela nyingi sana huwezi ukapanga bajeti yako ya kupambana na ugonjwa kama hauna takwimu huwezi ukajua wananchi wanateseka kiasi gani, takwimu ziwekwe wazi ili tafiti zifanyike", amesema Dkt. Mwaibambe
"Sisi kama Chama cha Madakatari tunaunga mkono kwa sababu yametoa mwanya kwamba iache sayansi ichukue mkondo wake", ameongeza Dkt. Mwaibambe