Kioja kilishuhudiwa eneo la Gatunga, Tharaka Nithi baada ya jeneza lililokuwa limebeba mabaki ya mzee wa boma moja kufunguka mara kadhaa na kukwama wenyeji walipojaribu kulipeleka kaburini.
Inasemekena, familia na wakazi walikuwa wamepuuza agizo la mzee huyo ambaye hakutaka mwili wake kuwekwa kwenye jeneza wakati wa mazishi.
Tharaka Nithi: Buda Azua Kisanga Baada ya ‘kudinda’ Kuzikwa
Mama seremala akitengeneza jeneza. Picha: TUKO.co.ke.
Kulingana na Taifa Leo, mzee huyo alikuwa akipendwa na wengi kutokana na ushauri wake nasaha na alikuwa nguzo na mfano mwema kwa wakazi licha ya kula chumvi nyingi kaisi cha kushindwa kutembea.
Inaarifiwa kwamba baada ya mzee kubaini kuwa siku zake zake duniani zilikuwa zinakamilika aliwaita jamaa wa familia yake na kuwaarifu kwamba mwili wake usiwekwe katika jeneza atakapoaga dunia.
Badala yake buda alitaka hela za kununua jeneza lake zitumike kuwafaidia waliolemewa na shida kijijni.
“Ninajua wanakijiji watatoa michango mbali mbali kutokana na upendo walio nao kwangu. Sitaki mjipe gharama ya kunivalisha suti mpya wala kununua jeneza la bei. Mnivishe mavazi yangu ya kawaida na blanketi iwe jeneza,” mzee alieleza.
Duru zinaarifu kuwa waliopokezwa ujumbe kutoka kwa mzee walikataa kushawishika na baada ya kifo chake kama ilivyotarajiwa wengi walichanga maelfu ya pesa ili kumfanyia mazishi ya kiheshima.
Walipuuza ujumbe wa mzee na kumnunulia suti ya kupendeza na jeneza la bei ghali.
Penyenye hata hivyo zinasema kuwa mipango ya mazishi ya mzee ilikuwa shwari hadi pale ambapo muda wa kumpuzisha ulipowadia.
Inasemekena kuwa waombolezaji walisimulia jinsi jeneza la mzee lilifunguka mara kadhaa na kukwama kila walipojaribu kuliingiza kwenye kaburi.
Baada ya kujaribu mara kadhaa na kufeli, ilibidi watii maagizo ya marehemu na kufanya alivyokuwa ameeleza kabla ya kifo chake.
Waliuondoa mwili wake ndani ya jeneza, wakamvisha mavazi mavazi ya kawaida kabla ya kurejesha jeneza hilo kwa muuzaji na kupewa pesa zao ili zikawafae maskini jisni alivyoagiza buda.