WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Mkaguzi Mkuu, Mkaguzi Msaidizi pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma zinazowakabili.
Akizungumza katika Kikao Kazi na Waziri wa Fedha na Mipango, Kaibu Mkuu, Manaibu Katibu Wakuu na Watendaji Waandamizi wa Wizara hiyo kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma Mei 27, 2021, Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna wa Polisi CP Salum Rashid Hamdun kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma hizo na ikithibitika kwamba tuhuma si za kweli wahusika watarejeshwa kazini.
Majaliwa amezitaja tuhuma hizo kuwa ni malipo yaliyofanyika Machi 31, 2021 kupitia vocha 30 ya Sh251 milioni yakielezwa kuwa ni malipo maalum bila kutaja kazi iliyofanywa na waliofanya kazi hizo. Taarifa hiyo imemnukuu Majaliwa akisema Sh155 milioni zililipwa kwa baadhi ya watumishi zikiwa ni posho yakuandaa miongozo wakazi.