Mashabiki wapatao 200 wa Manchester United wamevamia katika eneo la kuchezea (pitch) la uwanja wa Old Trafford kuendeleza maandamano ya kupinga umiliki wa familia ya Glazer katika klabu hiyo
Tukio hilo limefanyika mapema jioni hii ya leo Jumapili Mei 02, kabla ya mchezo wa Ligi kuu ya England dhidi ya Liverpool ambao ulipangwa kuanza majira ya saa 12:30 jioni ya leo.
Mashabiki hao tayari wameondolewa uwanjani na kikosi cha ulinzi na wengine kuamua kuondoka kabisa uwanjani hapo na kurudi majumbani kwao. Pia kulionekana kuwa na maandamano mengine nje ya hoteli ambayo wachezaji wa Man.United walipumzika kabla ya kuelekea uwanjani kwa ajili ya mchezo huo.
Maandamano hayo yamekuja baada ya uamuzi wa wamiliki wa United, pamoja na vilabu vingine vitano vya Ligi Kuu ya England, kujiunga na European Super league mapema mwezi uliopita kabla ya vilabu vyote kujitoa katika mashindano hayo.
Mwamuzi wa mchezo huo Michael Oliver na nahodha wa zamani wa Man.United Gary Neville walikuwa miongoni mwa wale ambao magari yao yalizingirwa na mashabiki walipokua wanaingia uwanjani, lkini hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya watu kujeruhiwa wala uharibifu wa mali.
Kwa mujibu wa Sky Sports, mchezo huo utachelewa kuanza ili kuhakikisha hali ya usalama inakuwa sawa katika mazingira ya uwanja.