MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Jacqueline Msongozi ameomba kupanda juu ya meza akiwa kwenye ukumbi wa Bunge ili kuieleza dunia kuwa wakulima hawataki mfumo wa stakabadhi ghalani kwenye mazao madogo ikiwemo ufuta.
Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo mwaka 2021/22 jana Jumanne Mei 25, 2021, Msongozi amesema mfumo huo haufai kwa mazao madogo.
Amebainisha kuwa wakulima wa Ruvuma wanalima ufuta kwa ajili ya kujikimu lakini kupitia mfumo huo hutakiwa kupeleka mazao katika mfumo wa stakabadhi ghalani na kukopwa jambo linalosababisha wakose fedha za kugharamia mahitaji yao.
“Spika (Job Ndugai) niruhusu nipande juu ya meza, niruhusu nipande juu ya meza sasa hivi,” amesema Msongozi na Ndugai kulazimika kumtuliza akisisitiza kuwa leo kitaeleweka kuhusu mfumo huo.
“Usipande mheshimiwa Jacqueline kwa sababu lazima leo kieleweke hapa kuhusiana na mfumo wa stakabadhi ghalani,” amesema Spika Ndugai.