Mishahara ya Wafanyakazi kuongezwa mwakani




Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan amesema licha ya matamanio yake ya kuongeza mishahara, Serikali haiwezi kufanya hivyo kwa sasa kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Hata hivyo, mkuu huyo wa nchi ameahidi kuongeza mishahara wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi  Meimosi, mwaka 2022.

Ili kutekeleza ahadi hiyo, Rais Samia ameagiza kuundwa mara moja kwa bodi ya mishahara itakayomwezesha kufahamu kiwango cha kuongeza katika mishahara ya watumishi wa umma na sekta binafsi.

Ameeleza hayo leo Jumamosi Meimosi, 2021 Mkoa wa Mwanza katika maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi ambayo kitaifa imefanyika mkoani humo.

Huku akiwaomba radhi wafanyakazi kwa kutokidhi kiu yao ya ongezeko la viwango vya mishahara, Rais Samia amesema inaumiza kuona wafanyakazi hawajaongezwa mishahara kwa kipindi kirefu na anatamani kuongeza lakini hali halisi inamkwamisha.

Ili kuwapunguzia machungu wafanyakazi, Rais Samia amesema Serikali imepunguza kodi na tozo  mbalimbali katika mishahara ya wafanyakazi.

''Nataka niwaambie kwamba serikali imesikia ombi la wafanyakazi la kutaka kupunguza kodi inayokatwa kwenye mishahara, tumeamua kupunguza asilimia moja ya makato ya Payee kutoka asilimi 9, mimi na nyinyi wote sasa tutakatwa asilimia 8," amesema Rais Samia

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad