KUNA methali moja ya Kiswahili isemayo; “Hakuna anayemshinda mwanaume kama mwanamke!” Hii imedhihirika katika Soko la Memorial mjini Moshi mkoani Kilimanjaro hivi karibuni kwa mwanamke ambaye alifahamika kwa jina moja la Elizabeth kuchezea kichapo kutoka kwa wafanyabiashara wanaume waliokuwa na hasira kali waliomkamata akiiba.
Mwanamke huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 42, alichezea kichapo hicho baada ya kujifanya mjamzito wa miezi nane mbele ya wanaume waliomkamata akiiba.
Kwa mujibu wa mashuhuda, Elizabeth alijifanya kuwa na ujauzito huo unakaribia kwenye hatua za mwisho, lakini baadaye aliumbuka baada ya kubainika kuwa aliutengeneza ujauzito huo. Aliposachiwa, alikutwa na tochi, kisu kidogo na karata za kuchezea.
Utata ulizidi kuhusu ujauzito wa mwanamke huyo baada ya mwanamke mmoja, mjasiriamali na aliyesomea masuala ya utabibu kwenda na kumchunguza kwa dakika chache na kubaini kuwa hakuwa na ujauzito.
Tukio hilo lilianza hivi; baada ya mwanamke huyo anayesemekana ni mkazi wa Kibosho alipoingia sokoni hapo mapema na kuongozana na vijana wanaobeba mizigo kwa matoroli na alipofika katika mojawapo ya meza ya mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Dominika Temba (24) almaarufu Mama Samir alimtaka kijana aubebe mzigo na kwenda nao nje ya lango.
Wakati hayo yakifanyika, mlinzi wa soko aliyejitambulisha kwa jina la Mudy alisema alimshtukia mwanamke huyo na kumuuliza kuhusu mzigo huo.
“Nilimshtukia, mimi ni mlinzi, ninawafahamu wenye meza na mizigo yao; sasa nilipomuona nikamkimbilia kumuuliza kwani vijana hawa wa Kimasai (wabeba mizigo) wengine siyo wazoefu na soko hili; akanijibu hapana hapo ndipo ngoma ilipoanza,” alisema mlinzi Mudy.
Mlinzi huyo alithibitisha kumkuta mwanamke huyo mwizi na karata, kisu kidogo na tochi na alipoanza kumsachi ndipo mwanamke huyo alipojifanya kuzidiwa na ujauzito ambapo Mudy alijivika ujasiri na kutaka kuthibitisha kama kweli ni mjamzito, lakini akaona mambo siyo kama alivyotegemea.
“Niliamua kumsachi kwa nafasi yangu kama mlinzi na kumhoji kama kweli ni mjamzito na sokoni amekuja kutafuta nini, akanipa mkanda wote kuwa ni shida tu zimemfanya afikie hapo na siyo kwamba ni mjamzito, ukubwa wa tumbo lake akaniambia kuwa alirogwa na ndugu zake, hivyo huonekana kama mjamzito,” alisema Mudy.
Hata hivyo, mwanamke huyo alipoona watu wanazidi kuwa wengi, alijifanya kuzidiwa kiasi cha kushindwa kunyanyuka kutokana na ujauzito wake ambao uliwahadaa wanaume waliokuwa na jazba ili wamtandike vibao kwa kusema ukweli.
Wanawake wajasiriamali sokoni hapo walipoona wanaume hao wanataka kutoa kichapo hicho walimzingira mwanamke huyo na walishauriana kumpeleka hospitalini kwa kuchangishana pesa ambapo kilipatikana kiasi cha shilingi 10,000 kwa ajili ya usafiri.
Wanaume walikataa wazo la kuchangia kwani walidai mwanamke huyo ni mwizi kama wezi wengine na angetakiwa kufikishwa Polisi kwanza kwa ajili ya kujieleza huku wanawake wengine walitaka jambo hilo limalizike sokoni hapo kwa maana mzigo umekamatwa salama ili kukomboa wakati katika utafutaji wa pesa.
Ilichukua takriban saa mbili na nusu kumuona Ofisa wa Jeshi la Polisi mwanamke ambaye alifika katika tukio hilo baada ya juhudi zilizofanyika na viongozi wa Soko la Memorial ili kunusuru maisha ya mwanamke huyo mwizi.
Makamu Mwenyekiti wa Soko la Memorial, Jeremia Adram alisema kuwa, wezi katika soko hilo wamekuwa wakitumia vijana wa Kimasai kuwarubuni kwa kiasi kidogo cha pesa kisha kuingia nao ndani kubeba mzigo ambao tayari walishaufanyia utafiti na kutokomea nao nje.
“Kama uongozi wa soko tunaendelea kuimarisha ulinzi huku tukiendelea kubaini mbinu chafu za wezi katika soko letu, Wamasai wasio na nia njema wamekuwa wakirubuniwa na wezi kwa pesa kidogo katika zoezi hilo, huyu mwanamke ni somo kwa wengine wenye tabia hiyo,” alisema.
Kwa upande wake, Mama Samir alisema; “Ningependa suala hili limalizike hapahapa, lakini kwa sababu limefika kwenye vyombo vya sheria, basi lakini nimetoka kukata beli jana, beli ambalo nimelinunua kwa laki nne na nusu hata laki sijauza mambo haya yanajitokeza, imeniuma sana.”
STORI: JABIR JOHNSON, MOSHI