WANAWAKE wasio na waume wanabaguliwa na wamiliki wa nyumba za kupangisha mjini Lagos, lakini hakuna changamoto inayokosa ufumbuzi. Idongesit Udoh alipowasili mjini Lagos na kuanza kazi yake mpya, rafiki zake walimtahadharisha kwamba kutakuwa na haja ya kutumia ujanja kidogo ili aweze kupata nyumba.
“Waliniambia kwamba nitahitaji kutafuta mwanamume ambaye pengine ni mjomba, binamu au rafiki yangu ili niweze kufikia makubaliano ya kupata nyumba na mwenye nyumba au wakala moja kwa moja,” anasema. Soko la nyumba mjini Lagos lina wateja wengi lakini linaendeshwa kwa mfumo dume; kwa ujumla wenye nyumba hawapendi kupangisha wanawake ambao hawajaolewa.
Hiyo, Udoh, 36, mhasibu mkuu katika kampuni moja ya kutoa ushauri, alilazimika kutumia njia ya mkato kwa kutafuta mwanaume ambaye alijfanya kuwa na uhusiano naye wa muda mrefu na akafanikiwa kupata nyumba, na kilichofuata ikawa na mwanamume yule kujiondoa taratibu wakati ameanza maisha yake.
“Huwa wanahakikisha wanakuwepo kwa kipindi cha kama mwezi, miezi miwili, mitatu, sita. Hadi wanapo hakikisha kwamba wamejenga dhana ya kwamba wapo, sasa wanaanza kujipoteza taratibu,” Udoh anasema. “Unaweza kujidai kwamba sasa mumetalikiana.”
Unyanyapaa dhidi ya wanawake ambao ni waseja
Mji wa Lagos una idadi kubwa ya watu na na mahitaji ya soko la nyumba hali inayowapa nguvu wamiliki au mawakala. Wengi wanachukua kodi ya mwaka mzima mara moja pamoja na ada ya wakala. Lakini kulingana na hitaji lilivyo, ina maanisha kwamba mwenye nyumba anaweza kukataa ombi la anayetaka kukodi ikiwa hajafikisha viwango alivyoweka.
Licha ya kwamba mji huo una kazi zinazolipa mshahara mzuri, wamiliki wengi wa nyumba hasa ‘Baby Boomers’ waliozaliwa baada ya Vita ya Pili ya Dunia ambao sasa hivi wako kwenye umri wa miaka 57-75 na kizazi cha Gen X waliozaliwa kati ya 1965 na 1979/80 ambao sasa hivi ni kati ya miaka 41-56 hawaamini kuwa wanawake wanaweza kumudu kodi ya mwaka mzima.
Wengi pia wanafikiria kuwa wanawake ambao hawajaolewa wanastahili kuishi na wazazi wao hadi watakapoolewa. Na ikiwa wamiliki wa nyumba watakubali kuwapangisha, wanapendelea kuwepo na mwanamume ambaye atakuwa kama dalali hata kama mwanamke ndiye anayejilipia kodi yake mwenyewe.
Afisa ustawi wa jamii Damilola Olushola sasa hivi anatafuta chumba cha kukodi karibu na kazini kwake lakini mwanamke huyo, 32, ambaye hana mume amekuwa na changamoto kupata nyumba.
“Nataka kuhama eneo la pwani ninaloishi kwasababu ya foleni ndefu lakini haijakuwa rahisi. Nimekuwa nikitafuta nyumba tangu Desemba nikifikiria kwamba nitafanikiwa kabla ya Machi lakini hadi sasa, bado natafuta,” amesema.
Hakuwa na bahati kwa sababu mmiliki wa nyumba anayoishi alikuwa anamshinikiza kuondoka kwa sababu mkataba wake unakamilika na kawaida ukitaka kuendelea na mkataba lazima ulipe kodi ya mwaka mzima badala ya mwezi mmoja. Na moja ya yale ambayo Olushola amehitajika kufanya ni kuongeza bajeti yake wakati anaendelea kutafuta nyumba karibu na kazini lakini anaona wenye nyumba wanachagua sana nani wa kumkodisha.
“Wakati mwingine ukiwa njiani na wakala anaanza kukupa masharti ya mwenye nyumba. Hataki mwanamke ambaye hajaolewa, au kama hajaolewa awe na mchumba. Kuna masharti mengi sana, mara hakuna kuingia usiku.”
Na kutokana na changamoto ambazo amepitia sasa anafikiria kumtafuta mwanamume ambaye watakubaliana amtumie kutafuta nyumba. “Mkuu wangu kazini ambaye ni mwanaume anafikiria kunisaidia tutafute nyumba pamoja. Pengine wenye nyumba watamuheshimu yeye … Nimechoka na desturi hii.”
Kwa kesi ya Udoh, aliyekuwa mchumba wake ambaye alijifanya kuwa mume wake na kumsaidia kupata nyumba, waliachana wiki moja baadaye. Na baada ya mmiliki wa nyumba kujua ukweli kwamba alitumia mbinu ya kijanja kupata nyumba, alimtimua na akalazimika kuanza tena mchakato wa kutafuta nyumba.
Wanaokodisha nyumba mara nyingi kuwa wanalaumu mawakala mambo yanapokwenda mrama lakini hawawezi kuwashawishi wamiliki katika uamuzi wao mwisho. Ugonma Arhuere, mjasiriamali ambaye anahusika na masuala ya nyumba anasema ni mchango kidogo sana unaotoka kwa wakala katika kumsaidia kupata nyumba.
Cha ajabu ni kwamba katika soko hilo, wanawake ambao hawajaolewa, waliotalakiana na wenza wao, waliofiwa na waume zao na hata wale ambao wameolewa lakini waume zao wanaishi maeneo ya mbali kwengineko, wote wanapitia kipindi kigumu kupata nyumba.
Tatizo ni kwamba, Arhuere anaeleza, wamiliki wa nyumba wanahisi kwamba wanawake ndio wanaoleta matatizo mengi mno, na wengi huwa na wasiwasi kwamba wanawake wanaoishi peke yao huenda ni makahaba na wanaweza kuwa na tabia ya kuleta kila aina ya wanaume majumbani mwao.
Na kufikia hapo, ni dhahiri shahiri kwamba utamaduni na dhana hii, ni ubaguzi na vinatakiwa kutokomezwa tena kwa haraka mno la sivyo, wanawake zaidi wataendelea kuishi wakiwa na msongo wa mawazo, ameongeza.
Suluhisho
Siku za hivi karibuni kumeibuka kampuni za kusimamia nyumba ambazo zinalipisha kodi kwa mwezi kama vile kampuni ya ‘Spleet’ iliyoanzishwa mwaka 2017 na ambayo sasa hivi imefungua ofisi zake katika maeneo mengine ya jangwa la Sahara.
Rais wa kampuni hiyo Viktor Ikoyalor, anasema kawaida huwa wanaangalia taarifa za anayetaka kukodi na wanawake hakuna ukaguzi zaidi ya mchakato wa kawaida wanaopitia. “Wanawake wengi huwa wanabaguliwa katika utamaduni uliozoeleka wa kutafuta nyumba ambao unaegemea mfumo dume,” anasema.
Anasisitiza kuwa kampuni yake ina lengo la kutoa suluhisho bora na la heshima katika suala hilo, licha ya hali zao kindoa. Daniela Ajala, 33, mkurugenzi wa mipango mikakati alitangaza chumba cha kukodisha katika mtandao wa kampuni ya ‘Sleept’ na ikachukuliwa na wanawake wawili ambao walikuwa ndio wamehamia Nigeria kikazi.
“Kwa bahati nzuri sikulazima kutafuta nyumba mjini Lagos,” anasema, “lakini nasikia simulizi nyingi sana za kushangaza. ” Inakatisha tamaa sana kuona kwamba maombi ya wanawake yanakataliwa kwasababu wanaishi peke yao, au kwa kuzingatia jinsia yao.
Upatikanaji wa nyumba bado hauendani na hitaji la bidhaa hiyo hasa katika mji wa Lagos wenye idadi kubwa ya watu na hatimaye kumesababisha ukosefu. Hata hivyo, serikali ya Nigeria inawekeza katika usafiri wa treni na vivuko vya baharini kuunganisha maeneo yenye idadi ndogo ya watu ya viungani mwa Lagos na mji mkuu wa kibiashara kukabiliana na tatizo hilo.
Ingawa changamoto iliyopo ni kwamba, miradi hii itachukua muda mrefu. Na hiyo ndio sababu wapo wamiliki wa nyumba ambao watakuwa tayari kubadilisha utamaduni uliopo. Hao watakuwa wanatekeleza jukumu muhimu katika utengenezaji wa fursa mpya kwa wanawake wasio na waume.