IMEBAINIKA kwamba, aliyekuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi, bado ana mkataba na klabu hiyo unaotarajiwa kumalizika Juni 30, mwaka huu.
Mwambusi alikaimu nafasi hiyo baada ya Yanga kulivunja benchi la ufundi lililokuwa chini ya Kocha Mkuu, Cedric Kaze raia wa Burundi.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mwambusi alisema: “Nipo ingawa sionekani Yanga kama zamani kwa sababu kama benchi la ufundi limekamilika na mwalimu amekuja na watu wake, hivyo siwezi kuwepo kwa sababu hiyo.
“Lakini nipo Yanga, ukiangalia kuna vitengo vingi na viongozi wenyewe wamenipa kitengo kingine cha kukaa ili kushughulika na timu yetu.
“Bado nina mkataba na Yanga na utamalizika mwishoni mwa mwezi wa sita.”Spoti Xtra lilimtafuta Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa kuzungumzia suala la Mwambusi na nafasi gani anashika kwa sasa ndani ya kikosi hicho, alisema:
“Mkataba wake kweli unaisha Juni 30, na alipewa mkataba wenye kipengele cha kuachia benchi pindi benchi jipya likipatikana.“Tayari benchi jipya limepatikana ndiyo maana yeye hayupo.”
STORI: LEEN ESSAU,DAR