Mwanafunzi Aeleza Alivyomsingizia Mwalimu Ujauzito




Rombo. Mwanafunzi wa kidato cha tatu (17), Shule ya Sekondari Ngareni ameeleza namna alivyomsingizia ujauzito mwalimu wa taaluma licha ya mimba hiyo kupewa na mzee wa miaka 70 (jina tunalihifadhi).

Hata hivyo, mwalimu wa taaluma Shule ya Sekondari Ngareni, Hemed Said alisema anamshukuru Mungu mwanafunzi huyo kuamua kusema ukweli, kwa kuwa jambo hilo lilimchafua sana.

“Mimi nina familia, isitoshe ni mwalimu wa taaluma katika shule hiyo, imani ya wazazi ilipungua kwangu na imeniathiri kwa kiasi kikubwa,” alisema Mwalimu Said.

Aliviomba vyombo husika vifanye uchunguzi wa kina na kuweka ukweli wazi ili sintofahamu kama hiyo isitokee tena kwa mtu mwingine.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Amon Kakwale alilieleza Gazeti la Mwananchi kuwa mzee huyo ambaye ni mgambo anashikiliwa na polisi kwa ajili ya uchunguzi.

Kakwale alisema kutokana na unyeti wa suala hilo, lazima vipimo vya vinasaba vifanyike ili kubaini ukweli, “na tayari tumeshafanya mawasiliano na wahusika ili kujua gharama.”

Akizungumza na Mwananchi katika Hospitali ya Ngoyoni alikokwenda kujifungua, mwanafunzi huyo alisema Desemba 12, mwaka jana aligundua kuwa na ujauzito na kusababisha kukatisha masomo yake.


Alidai baada ya kugundua hivyo alimweleza babu huyo ambaye ni baba mkwe wa shangazi yake aliyekuwa akiishi naye kuwa ana mimba yake.

Mwanafunzi huyo alisema baada ya kumweleza, babu huyo alitaka kujua ina muda gani.

Alidai baada ya kumjibu kuwa hajui alimpeleka hospitali ya wilaya hiyo na kubainika mimba hiyo ilikuwa ya miezi minne.

“Babu alinipeleka hospitali ya Wilaya Huruma, tukiwa njiani ananirudisha nyumbani akaniambia nisema ujauzito ni mwalimu wangu wa darasa, jambo ambalo nilikubali,” alisema mwanafunzi huyo.


“Baada ya kuniambia hivyo, alisema nikikataa hatonipa pesa za matumizi, hivyo ikanibidi niende kumweleza mwanafunzi mwenzangu kuwa mimi ni mjamzito na mimba ni ya mwalimu, kisha akaenda kupeleka taarifa hizo kwa mkuu wa shule yetu.”

Mwanafunzi huyo aliendelea kusema baada ya taarifa hizo kufika kwa mwalimu mkuu aliitwa na alipoulizwa alikiri kuwa na ujauzito na wa mwalimu wake wa taaluma.

“Nilisema hivyo kwa sababu babu aliniambia nimtaje mwalimu na nisimtaje yeye, endapo nikimtaja hatanisaidia kwa chochote,” alisema mwanafunzi huyo.

“Babu alikuwa akinipa Sh2,000 na kuninunulia zawadi ndogondogo, pia aliniahidi kunilipia fedha ya mahafali, ndio maana nilikuwa nikifanya naye mapenzi. “Alikuwa ananiambia niamke mapema nipitie dukani alikokuwa analala tunafanya yetu tukimaliza ananipa maji nanawa na kisha ananipeleka shule kwa usafiri wa pikipiki yake,” alisema mwanafuzi huyo.


Alisema baada ya kujulikana ni mjamzito shangazi yake alimfukuza na kwenda kuishi na mama yake mzazi.

Mama mzazi wa mwanafunzi huyo alisema mtoto wake aliamua kusema ukweli kwa kuhofia maisha yake wakati akijifungua.

Alisema baada ya mtoto kumweleza ukweli alikwenda kwa mwenyekiti wa kitongoji ili kupeleka taarifa hizo ili hatua mbalimbali za kisheria zichukuliwe.

Alisema mwenyekiti wa kitongoji alizipeleka taarifa kwa diwani wa kata hiyo ili aweze kuzifikisha kwa wakubwa zaidi na mtuhumiwa achukuliwe hatua.

Diwani wa Ngoyoni, Felisian Kavishe alisema mwanafunzi huyo alishinikizwa na babu yake kumtaja mwalimu wake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad