Spika wa Bunge, Job Ndugai leo Ijumaa Mei 7, 2021 amesisitiza kuhusu wabunge 19 waliofukuzwa uanachama Chadema, akitaka kupatiwa vielelezo kuhusu kufukuzwa kwao na kwamba huo ni msimamo wa kiti.
Wabunge hao 19 akiwemo Halima Mdee walifukuzwa Chadema Novemba mwaka 2020 baada ya kuapishwa kuwa wabunge bila ridhaa ya chama hicho lakini wameendelea kuwa wabunge jambo ambalo kwa nyakati tofauti Chadema wamelipinga huku Ndugai akidai hana vielelezo.
"Hata akija Spika mwingine bado msimamo utakuwa ni huohuo, lazima kuwepo na viambatanisho ili na mimi niwasiliane na msajili wa vyama vya siasa tujue kama kamati iliyotoa uamuzi ina haki au vinginevyo," amesema Ndugai.
Amesema angalizo hilo haliwalengi wabunge wa upande mmoja tu bali kwa chama chochote cha siasa ambacho kitakuwa na nia ya kuwatimua wabunge.
Leo pia amerejea kauli yake kuwa hayupo kwa ajili ya kufukuza wabunge bali kuwalinda.