SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai amesema wapo wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ambao wamekuwa wakijiita marais wa mikoa jambo ambalo linawafanya kujiona ndio kila kitu kwenye mikoa/wilaya hizo na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Ndugai amesema hayo leo Jumatano, Mei 19, 2021 wakati akitoa pongezi kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa taasisi walioapishwa na Rais Samia Suluhu, Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Kumekuwa na maonezi makubwa sana katika Taasisi ya TAKUKURU, sisi tunaowakilisha wananchi tunaona, si vizuri kuwaonea watu haipendezi hata kidogo, si mahali pa kusema lakini Waziri atawaeleza.
“Kuna wakuu wa mikoa ambao sisi kama Bunge huwa tunakutana nao, lakini baadhi yao kuna mambo yanawafnyika kwenye mikoa yao mkiwaambia wanashangaa, haipendezi wewe mkuu wa mkoa unakuja unashangaa Bungeni na hujui kinachoendelea mkoani kwako.
“Wakuu wa mikoa na viongozi wengine wa mikoa tufanye kazi kama timu, sio muwaachie wakurugenzi pekee, sheria hazijatungwa kwa ajili ya Wakurugenzi pekee, hivyo likiharibika jambo wote muwajibike, pesa inatengwa, jambo linafanyika na wewe RC hujui.
“Wapo Ma-RC, Ma-DC huko nyuma sio nyinyi walikuwa wakisema mimi Rais wa mkoa huu mimi ni DC wa wilaya hii, nani kakudanganya? Rais ni mmoja tu, Samia Suluhu basi. Ukijivisha urais huko uliko unafanya mambo ukidhani kwamba wewe ni Rais.
“Utengenezwe utaratibu wa viongozi kuwajibika kwa pamoja yaani Mkuu wa mkoa, Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi maana haiwezekani jambo likiharibika linakuwa la Mkurugenzi pekee, hawa wengine wana-relax,” amesema Ndugai.