Ndugu Wanyofoana Midomo Wakigombea Urithi Wa Mama






NDUGU wanaozaliwa na mama mmoja, baba tofauti Juma Nsenga na Yohana Makire, wakazi wa Kitongoji cha Msati Kata ya Sabababa, Mkoa wa Mara wameng’atana na kujeruhiana midomo na pua wakigombea urithi wa makazi yaliyoachwa na mama yao aliyefariki mwaka jana.


Juma alimng’ata Yohana na kumjeruhi mdomo wa chini wakati Yohana naye alimng’ata kaka yake huyo mdomo wa chini mpaka akaondoa kipande na kukitema, kisha akang’ata pua ya upande wa kulia na kuimega kipande na kukitemea kando.



Kufuatia ugomvi huo kaka yao anayeitwa Kawawa Nsenga alifikisha mgogoro huo kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la Kata hiyo, akiomba liingilie kati kusaidia mgawanyo wa eneo hilo ili kila mmoja apate kipande chake na kukitumia bila kubugudhiwa na yeyote.



Akitoa ushahidi kwenye Baraza hilo ambalo limefikia hatua ya kukusanya ushahidi, Kawawa alisema alifungua shauri hilo kutokana na picha ya wanaukoo aliyoipata wakati wa kikao cha familia, pamoja na hulka ya mhemko waliyonayo wadogo zake hao.



“Sikuja kugawa ndugu zangu kwamba huyu atoke, huyu abaki, bali tusaidiwe ili kila mmoja kati ya hawa ndugu apate kasehemu



kake,” alisema Kawawa.



Alisema kiwanja hicho kilipatikana kutokana na mahari iliyolipwa kwa ajili ya dada yao (bila kutaja jina), tofauti na madai ya baadhi ya mashahidi.



Awali Baraza lilielezwa na baadhi ya mashaidi akiwamo jirani Radislaus Frowino, kuwa mara mbili alishuhudia Juma akimpiga mama yake na kwamba alilazimika kumchukua mama huyo nyumbani kwake na kufanya mazungumzo naye, ili kujua kiini cha tatizo.



“Mama yao alisema alikuwa akifanyiwa fujo ikiwamo kupigwa na Juma kutokana na uchochezi wa kaka yake Kawawa, ambaye alitaka akimbie ili wauze uwanja (makazi) wake na yeye alikusudia kumpatia kijana wake mdogo



(Yohana) ambaye ndugu zake walikuwa wakimtenga wakisema ni mtoto wa nje ya ndoa,” alisema Frowino ambaye kitaaluma ni Mwalimu.



Alisema waliafikiana ampeleke kwa mwanasheria ili aandike wosia, kutimiza azma yake ya kuacha makazi hayo kwa Babu (Yohana) endapo ingetokea akafariki, lakini kabla hawajatekeleza hayo mama huyo alifariki.



Mdogo wa marehemu, Zainab Rashid alisema akiwa hai dada yake alikuwa akipeleka malalamiko kwa ndugu zake akiwamo yeye kwamba watoto wake wakubwa walikuwa wakimtenga Yohana na kwamba hata ikitokea akafa makazi hayo ni ya mtoto huyo.



“Huu uwanja ni wa Babu(Yohana), alipewa na Deus Makire ambaye aliukabidhi kwa ghati ili amtunzie mtoto wao,” alisema.



Yohana alisema wakubwa zake hao walizaliwa wilayani Serengeti na wana baba yao ambaye aliachana na mama yake kabla hajahamia Tarime ambako alikutana na baba yake(Yohana) hatimaye na yeye kuzaliwa.



Alisema baadaye ndugu zake hao walianza kwenda nyumbani hapo mmoja baada ya mwingine, aliwataja kuwa ni Kawawa Nsenga, Bhoke Nsenga, Juma Nsenga na Mkami Nsenga.



Hata hivyo hakuna upande wenye maandiko yanayoweza kuthibitisha madai hayo na shauri hilo liliahirishwa na Mwenyekiti wa Baraza, Nyamwita Marwa mpaka Jumanne, wiki ijayo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad