WAKATI makanisa na baa zilifungwa kote nchini Kenya kwa sababu ya COVID-19, Mhubiri Ken Baraza wa Kanisa la Abundant Grace Revival Ministries alikuwa anafunga na kumuomba Mungu ampe neema ya kubadilisha eneo moja la burudani mjini Kakamega kuwa mahali pa kuabudu.
Na kweli maombi yake yalijibiwa kwani alifaulu kubadilisha (Night Club) klabu ya Scotch Baron Lounge kuwa kanisa. Pasta Baraza alielezea kwamba alikuwa amelenga kuibadilisha baa ya Scotch Baron Lounge, ambayo ni sehemu ya burudani mjini Kakamega, kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa ripoti ya The Standard, Baraza alisema haja yake ilikuwa kuwavizia watu wengi kumkubali Yesu Kristu kupitia njia ya kipekee ambayo mapasta wengi wanaogopa.
Mabadiliko hayo ya ghafla yaliwaduwaza wengi ambao walikuwa wamejipanga kujiburudisha kwenye klabu hiyo wikendi huku wakishangaa mahali wanapopenda paligeuzwa kuwa pa kuabudu.
“Mara ya kwanza nilifikiri ilikuwa mchezo hadi kanisa hilo lilipoanza kwa vishindo,” alisema mmoja aliyependa klabu hiyo.
Mhubiri huyo pia alifichua kuwa aliwahi kubadilisha baa moja kuwa kanisa katika eneo la Ndumberi kaunti ya Kiambu mwaka 2004.
“Haikuwa rahisi, ilituchukua miezi kadhaa kukataliwa na majadiliano kufaulu,” alisema. Jengo hilo sasa linajengwa upya kubadilishwa kutoka baa hadi kanisa.
“Lengo letu kuu ni kuleta nuru ambapo kuna giza.Tunakemea roho za giza na sio mtu binafsi, tunawakumbatia walevi ambao wanataka kujiunga na kanisa letu,” aliongezea.
Mhubiri huyo alisema huwa analenga baa katika misheni yake kwa sababu ya kukulia katika familia ya walevi. “Ninatoka kwa familia ya walevi. Kila mtu alikuwa anakunywa ikiwemo dada zangu. Kwa neema ya Mungu niliepuka tabia hiyo,” alisema.