Rais Hussein Mwinyi Mgeni Rasmi Uzinduzi Wa Mbio Za Mwenge Wa Uhuru 2021

 




Na: Mwandishi Wetu – Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo kitaifa zitazinduliwa Uwanja wa Mwehe – Makunduchi, Mkoani Kusini Unguja, Zanzibar.


Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokutana na Waandishi wa Habari kwenye Ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kwa lengo la kutoa taarifa kwa umma kuhusu tukio la uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2021..


Mheshimiwa Mhagama alisema kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu wa 2021 ni Mbio maalum, umaalum wake pia unatokana na Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru kukimbizwa katika Wilaya 150 za kiutawa tu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania badala ya Halimashauri za Wilaya 195 kama ilivyozoeleka.


“Chombo hiki sasa ni budi kikimbizwe tena nchini kote baada ya kutofanya kazi toka mwaka 2020 kutokana changamoto za Ugonjwa wa Corona, hivyo ili kiweze kurejesha matumaini kwa watanzania na kuwahimiza kuchapa kazi chini uongozi shupavu wa Serikali ya awamu ya sita inayoongwa na Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Mhagama


Alifafanua kuwa, Falsafa ya Mwenge Mwenge wa Uhuru ndio chimbuko la Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Mwaka 1964 na Azmio la Arusha la mwaka 1967.


Akinukuhu maneno ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoyatoa mwaka 1958 wakati akihutubia kikao cha 35 cha Umoja wa Mataifa na kuyarudia tarehe 22 Oktoba, 1959 wakati akihutubia Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika (LEGCO) “Sisi watu wa Tanganyika, tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pamejaa chuki na heshima palipo na dharau”


“Ni mwaka wa 29 sasa toka Mbio za Mwenge wa Uhuru zilivyoanzishwa na waasisi wetu na umeendelea kuwa chombo muhimu kwa Taifa kwa kujenga undugu, umoja, mshikamano na kudumisha amani pote unapopita bila kujali itikadi zetu za kisiasa, dini wala makabila yetu.” alieleza


Aliongeza kuwa Mwenge wa uhuru na mbio zake zimekuwa na faida kwa taifa ikiwemo kuendelea kuhamasisha Wananchi kushirikiana na Serikali yao katika kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali za maendeleo katika nyanja za kilimo, ufugaji, Uvuvi endelevu, uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, elimu, maji, umeme na huduma za jamii katika maeneo yote nchini na hasa katika maeneo yasiyofikika kiurahisi.


Pia Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru zimekuwa zikitumika kuelimisha wananchi katika maeneo yote nchini jinsi ya kupambana na maradhi yanayotishia ustawi wa watu wetu kama vile UKIMWI, Malaria na kuhamasisha wananchi kushiriki vita dhidhi ya Rushwa na matumizi ya Dawa za kulevya na sasa zitaichukua dhana ya Lishe bora kwa afya Imara ya Watanzania. Pamoja na njia nyingine tunazotumia kuwahamasisha wananchi wetu. Bado Mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa ni njia sahihi ya kufikisha taarifa na elimu sahihi ya changomoto zinazowakabili watanzania wote.


Aidha, Waziri Mhagama alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi wote wa Zanzibar, kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Mwehe   Zanzibar na kuungana na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kufanikisha shughuli muhimu kitaifa.


Kwa Upande wake, Kaimu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Leila Mohamed Mussa alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamefanikiwa kukamilisha maandalizi kwa asilimia 100.


“Watendaji wa Serikali zote mbili wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ufanisi wa uzinduzi hu una hivyo Mwenge huo kuanza kukimbizwa rasmi” alisema Mheshimiwa Leila


Alitumia pia fursa hiyo kuwaalika wakazi wa Makunduchi na maeneo mengine mbalimbali kujitokeza kwa wingi.


Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2021, unahusu matumizi sahisi ya TEHAMA, chini ya Kauli mbiu isemayo: “TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu .Itumie kwa usahihi na Uwajibikaji”. Pamoja na Ujumbe huo, Mbio za Mwenge wa Uhuru zitaendelea kuwakumbusha na kuwahamasisha wananchi na Viongozi kote nchini, kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI, ugonjwa Malaria, mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za Kulevya, Mapambano dhidi ya Rushwa na kuhamasisha Wananchi juu ya Lishe bora kwa afya imara.


MWISHO

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad