Rais Samia Amzawadia Gari Mzee Mwinyi



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu amemkabidhi zawadi ya gari ya kutumia katika safari zake Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Mh. Alhaj Ali Hassan Mwinyi aliyonunuliwa na serikali katika uzinduzi wa kitabu chake jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia amesema; “Nakushukuru sana Mzee wangu Rais Mstaafu Mwinyi kwa kunikaribisha kuzindua kitabu cha simulizi ya maisha yako, nampongeza Mzee Mwinyi kwa kuamua kuandika kitabu ambacho sio tu kitawasaidia Watanzania na Dunia kumfahamu pia kina historia ya Tanzania.

 

“Shughuli ya uzinduzi wa kitabu hiki iilipangwa ifanywe na mtangulizi wangu Hayati Dkt. John Magufuli, mwezi Machi mwaka huu, hata hivyo kwa mapenzi ya Mungu hakuwahi kuifanya kazi hiyo.

 

“Kitabu chako nimekisoma mara 2, mara ya kwanza nilivyosoma niliyoyakuta ndani nikashtuka nikasema mtu wa maarifa na hekma zote kama Mzee Mwinyi yamempata haya mie je! Kikanipa woga kidogo, nilipokisoma mara ya pili uoga ukanitoka.

“Hafla ya uzinduzi wa kitabu cha Mzee Mwinyi inaenda sambamba na kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa, tunamtakia kila la kheri wakati anatimiza miaka 96, tunamuomba Mungu akutunze ili tuzidi kuvuna hekima na busara zako.



“Mzee Mwinyi alipelekwa Zanzibar kutayarishwa kuwa Sheikh mkubwa lakini kwa neema za Mungu akaishia kuwa Rais wa Tanzania, natamani kuelezea kitabu chote ila nahofia kitakosa wanunuzi ila yoyote atakayesoma atajifunza mengi binafsi nimejifunza mengi.

“Kikubwa zaidi nilichojifunza kwenye kitabu cha Mzee Mwinyi ni kwamba Mzee Mwinyi ni Baba wa Mageuzi, alipoingia madarakani Nchi yetu ilikuwa vibaya kiuchumi lakini alipoingia akafanya mageuzi, alianzisha ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma ikiwemo Kiwanda cha Bia.

“Mzee Mwinyi ndiye aliyesimamia kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi nchini kwahiyo ni sahihi kusema yeye ni Baba wa Mageuzi, pia Mzee Mwinyi ametufundisha kwamba Uongozi wa Nchi hautafutwi ila unakutafuta, alikuwa Rais bila kumuhonga Mtu wala kutumia nguvu.

“Mzee Mwinyi anasema alibinafsisha Kiwanda cha Bia Tanzania kwasababu kilikuwa kinaendeshwa kwa hasara, kabla ulikuwa ukitaka bia kwa ajili ya harusi ilikulazimu kupata kibali cha kununua bia kutoka kiwandani au kwa Wakala tena kwa kuonesha kadi za mialiko ya harusi.

“Tunafarijika sana kukuona ukiwa mwenye afya bila shaka inalisadifu jina lako la Nzasa yaani isiyokauka, lakini huenda ikatokana na tabia yako ya kutokopa kwa sababu kukopa kunatia hofu, wasiwasi, kunadhoofisha moyo na kunyima raha.

“Nimemuandalia zawadi Mzee Mwinyi, kwa kutimiza umri wa miaka 96 leo, nimekuwa nikiona usumbufu anaoupata akiwa anapanda na kushuka kwenye Gari lake, kwa niaba ya Serikali Mzee wetu leo tutampatia Benz la chini ambalo litampa raha kwenye safari zake.

“Alipata Urais bila kutumia nguvu wala kumhonga mtu yeyote hili ni funzo kubwa kwa wote wenye dhamira kuwa viongozi kwamba, mbali na mikiki yetu tunaposaka madaraka, uongozi na jambo lolote lile ni kwa kudra za Mwenyezi Mungu.

 

“Mzee Mwinyi ametufundisha kwamba uongozi ni dhamana, kama tulivyosikia 1977 akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alijiuzulu kwa hiari wakati wa mahojiano ya watuhumiwa wa mauaji ya vikongwe kule Shinyanga kwa imani za kishirikina.

“Kama mnavyojua leo ni siku ya kuzaliwa kwa Mzee wetu, nimemuangalia na kimo chake na usumbufu anaoupata wakati wa kupanda na kushuka gari tulilompa, tumeona tumpunguzie kadhia hiyo hivyo tutampatia Benz ya chini gari itakayompa raha,” amesema Rais Samia
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad