Rais Samia Apunguza Kodi ya Mishahara, Makato Bodi ya Mikopo






Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameongoza wafanyakazi mbalimbali katika Kilele cha Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi Kitaifa ambazo zimefanyika Jijini Mwanza leo Mei 1, 2021 katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.

Rais wa TUCTA Tumaini Nyamhokya amesema; “Wafanyakazi wamelia kwa muda sasa kuhusu suala la mishahara, tutashukuru endapo utatazama kwa namna moja au nyingine ili tuweze kupata nyongeza ya mishahara. Pia ikikupendeza tunaomba uliangalie suala la kodi ya PAYE (Pay as You Earn).”

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amemuomba Rais Samia aongeze mishahara ya watumishi wa umma “Mimi sitasema mengi, nina ujumbe wa wafanyakazi wanasema wanasubiri mama useme neno ili mioyo yao ipone. Nami sina shaka kwani ilani imeahidi masilahi bora ya watumishi.”

Aidha, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kimeishauri Serikali kufanya mapitio katika Sera ya Elimu ya 2014, kwa ajili ya kuboresha mitaala iliyopo ili iweze kutoa elimu ya ujuzi kulingana na soko la ajira.

Akizungumza wakati akitoa hostuba yake, rais Samia amesema mishahara haijaongezwa kwa wafanyakazi karibu miaka nane kwa sekta isiyo rasmi na miaka sita kwa sekta ya umma. Hali hii imepunguza molari ya wafanyakazi kufanya kazi.

“Mishahara haijaongezwa kwa muda mrefu, mimi binafsi natamani kuongeza mishahara mwaka huu ila kwasababu mbalimbali nimeshindwa, uchumi wa Tanzania umeshuka kutoka 6.9% hadi 4.7% kwasababu ya Corona, mwakani siku kama ya leo nitapandisha mishahara.

“Serikali imesikia ombi la kupunguza kodi ya mishahara yaani PAYE na tumepunguza asilimia moja kutoka tisa hadi nane. Mtakatwa ninyi pamoja na mimi.

“Makato ya bodi ya mikopo, kwenye changamoto hii tumeamua kubakia kwenye asilimia 15 ya sasa na serikali imefuta asilimia sita iliyokuwa ikikatwa. Lakini nasisitiza, waliokopa wahakikishe wanalipa. Serikali imeongoza umri wa mtegemezi kwa mtoto kutoka miaka 18 hadi 21. Maamuzi haya, tutayajumuisha kwenye mabadiliko ya sheria." Rais Samia amesema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad