Taasisi ya Kudhibiti Usalama wa Chakula ya Umoja wa Ulaya (EU) imesema matumizi makubwa ya rangi katika vyakula, ambayo huandikwa E171 katika sticker za vyakula, haitakiwi iendelee kuchukuliwa kama ni kitu salama kwa matumizi.
Rangi hiyo ya E171 inajumuisha vipande vya Kemikali ya Titanium Dioxide na inatumiwa sana katika bidhaa za walaji. Katika vyakula, kionjo hicho hutumika kuweka rangi nyeupe katika pipi, bazoka, mchuzi mweupe na katika keki ili kuifanya ionekane kama imezungushiwa barafu.
Lakini matumizi yake katika chakula yalizuiwa mwaka jana nchini Ufaransa kutokana na hofu za kiafya. Mamlaka ya Usalama wa Chakula ya Ulaya (EFSA) iliyo na makazi yake nchini Italia, imesema baada ya kuangalia upya ushahidi, kuna hatari kwamba vipandevipande vya titanium dioxide vinaweza kuharibu vinasaba (DNA), na kwamba hakuna kiwango salama kinachoweza kuwekwa kwa ajili ya matumizi ya kila siku.
“Kwa kuzingatia utafiti wote wa kisayansi na taarifa zilizopo, jopo limehitimisha kuwa titanium dioxide haiwezi tena kuchukuliwa kuwa ni salama kutumika katika chakula,” amesema Maged Younes, Mwenyekiti wa jopo la wataalamu la EFSA linaloshughulikia vionjo vya nyongeza katika vyakula.
Jukumu limebakia kwa Kamisheni ya Ulaya na nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kuamua kupiga marufuku matumizi ya rangi hizo.