Rais Samia Suluhu Hassan amewatumia salamu wahalifu hasa wa ujambazi ambao amesema wameanza kufanya matukio hayo, amewaonya wasijaribu kupima kina cha maji kwa mguu, amemuagiza IGP Simon Sirro kupambana nao haraka iwezekanavyo.
Rais Samia amesema hayo leo Ijumaa, mei 7, 2021, wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mlimani City na kusema kuwa ugumu wa maisha si chanzo cha uhalifu bali kuna sababu nyingine.
“Leo nimesoma mtandaoni, Dar es Salaam kuna Watu wanajaribu kupima kina cha maji, viujambazi vimeanza kuja juu, naomba nitoe meseji wasijaribu kina cha maji, IGP upo hapa, mitandaoni wanamtaja Afande mmoja alikomesha ujambazi, wanasema ‘Mama turudishie’, IGP kaliangalie hilo.
“Suala la wazee wote kuwalipa pensheni tulianza kulijadili serikalini tangu mwaka 2014 tukaona mzigo ni mkubwa sana, tukaenda angalau kuanzia miaka 70 bado mzigo ukawa ni mkubwa, sitaki kuwadanganya wazee wangu.’
“Corona imeshusha Uchumi karibu wa Dunia nzima. Sisi uchumi wetu umeshuka kutoka takribani asilimia 7 mpaka aslimia 4.7 hivi. Pamoja na kwamba tutajitutumua tukue lakini tuna miradi mikubwa ambayo inahitaji kukamilika. Naomba mnipe muda niangalie hali ya Uchumi inavyokua halafu nitalitolea maamuzi. Tujenge Nchi kwanza halafu tutagawana faida.
“Nitoe wito kwa Jamii ya Kitanzania tutunze Wazee iwe amekuzaa au hajakuzaa, tuna kisingizio cha maisha magumu ila naona ni maadili, shughuli ya kuchukua Wazee kuwaweka kwenye nyumba maalum inafanywa na wenzetu wa Magharibi, Serikali itawajengea nyumba ila tuwatunze.
Turudi kwenye malezi yenye maadili maalum, kwenye Mabasi ya Mwendokasi kuna viti vya Wazee na Wajawazito ila inashangaza kukuta Vijana wapo kwenye kiti Wazee wamesimama, pia niwaombe Makonda wahakikishe Mzee amepata kiti amekaa na amwambie Kijana mpishe Mzee,” amesema Rais Samia.