Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile amesema huenda wakaanzisha zoezi jipya la uhakiki wa laini za simu zilizosajiliwa kwa alama za vidole lengo likiwa ni kupambana na wahalifu mtandaoni.
Dk Ndugulile ameyasema hayo jana Jumatano Mei 19, 2021 wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia makadirio ya matumizi na mapato ya wizara yake.
Amesema wanakwenda kuboresha mifumo yao na kwamba Mei 26, 2021 yeye na mawaziri wenzake (hakuwataja) watakaa kuangalia njia bora, wanaweza kubana katika usajili wa simu ikiwa ni hatua ya kupambana na uhalifu huo.
“Tunaweza tukaja na zoezi jipya la uhakiki wa watu waliojisajili kwa alama za vidole ili kuhakikisha wote wenye kadi za simu wamesajiliwa na tunaweza kuweka mifumo ya kuweza kuwabaini,” amesema.
Amesema teknolojia wanayo ya kuangalia jinsi gani ya kuzifungia laini zinazotumika kwenye uhalifu.
Kuhusu vizimbuzi kutoonyesha chaneli za Tanzania, Dk Ndugulile amesema ametoa maelekezo kuwa wadau wa vizimbuzi na televisheni wakutane kujadili na maamuzi yoyote Serikali itayabariki.
Amesema wanataka kufanya mapinduzi makubwa hasa katika tasnia ya televisheni.
Pia, Ndugulile amesema sekta hiyo inakuwa kwa kasi na wanaenda kufanya maboresho ya sheria kikwazo kwa muda mrefu.
“Sitaki kukumbukwa kama waziri aliyekuwa polisi wa sekta nataka nikumbukwe kama waziri aliyeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya Tehama. Sitaki kuminya na kuwa polisi. Nataka nikumbukwe kama waziri aliyekwenda kufanya mazingira wezeshi ya sekta ya Tehama kukuwa ndani ya nchi,” amesema.
Bila kufafanua zaidi, Dk Ndugulile amesema kutokana na hilo anakwenda kufanya mabadiliko makubwa ya kimuundo ya taasisi na kisheria.
Ametoa mfano wa mabadiliko ya sheria ili vijana wanaojiajiri kupitia Tehama kutotozwa kodi.
“Kijana ni mshereheshaji anafanya shughuli za harusi anarusha picha zake kwenye Youtube ili aonekane kuwa ni imara na sisi tunakwenda kumtoza kodi. Sisi tunataka kuondokana nalo,” amesema.
Ametoa mfano mwingine wa wasanii wanaotengeneza nyimbo zao wanaweka mitandao kwa ajili ya kujipatia fedha halafu wao wanawaminya.
Amebainisha kuwa wataandaa mazingira wezeshi na si kuweka kizuizi ila kuhakikisha wasanii na vijana wanajiajiri kupitia Tehama.