Kiongozi mkubwa wa Kiislamu mashariki mwa DRC ameuawa kwa kupigwa risasi wakati akisali kwenye msikiti mkuu mjini Beni.
Mtu mwenye silaha alimfyatulia risasi Sheikh Ali Amini wakati wa swala ya Magharibi siku ya Jumamosi kisha akakimbia, mwanaharakati wa haki za binadamu ameeleza.
Kiongozi huyo alikuwa akikemea vitendo vya wanamgambo wa kiislamu kwenye eneo hilo, Shirika la habari la Reuters limeripoti.
Mashariki mwa Congo imekumbwa na hali mbaya ya usalama, ikiwemo mashambulizi yanayodaiwa kutekelezwa na kundi la wanamgambo wa Kiislamu (IS)
Kifo cha Sheikh Amini wakati huu wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani umesababisha mshtuko mkubwa mjini Beni, mji ulio na watu karibu 200,000.
Mwanaharakati mjini humo Stewart Muhindo, amesema kuwa tukio hili ni la kwanza kutokea mjini humo.
''Ilitokea wakati wa swala ya Magharibi. Risasi zilifyatuliwa ndani ya msikiti na kumpata Imam. Mtu huyo alitoka eneo la tukio, alikuwa na mwenzake ambaye alikuwa akimsubiri na pikipiki''. Bw. Muhindo aliiambia BBC.
Ingawa haijulikani ni nani aliyetekeleza shambulio hilo, ghasia nyingi katika eneo hilo zinafanywa na kundi la waasi la Kiislamu, Allied Democratic Forces (ADF), mwandishi wetu anasema.
IS imedaiwa kutekeleza mashambulio kadhaa ya ADF, lakini haijulikani makundi haya mawili yana uhusiano wenye nguvu kiasi gani.
ADF iliundwa zaidi ya miaka 20 iliyopita katika nchi jirani ya Uganda ili kupambana na madai ya ubaguzi dhidi ya Waislamu. Ilihamia mashariki mwa Congo baada ya kufukuzwa kutoka kwa vituo vyake na jeshi la Uganda.
Kundi hilo limeongeza mashambulizi dhidi ya raia tangu DRC ilipoanza vita dhidi ya kundi hilo mwezi Oktoba mwaka 2019.
Karibu watu 200 wameuawa na kundi la ADF tangu mwezi Januari. Umoja wa Mataifa umeeleza.