Simba Watamba ‘Hamtaamini’ Leo Uwanja wa Mkapa





MTASHANGAA na hamtaamini! Ndiyo maneno ambayo yatatumika leo pale Simba itakapokuwa ikiingia uwanjani kuwavaa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika mchezo wao wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Leo majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, Simba itashuka uwanjani mbele ya mashabiki zaidi ya 10,000 kuisaka rekodi ya kupindua meza kwa kupata ushindi wa tofauti ya mabao 5-0 dhidi ya Kaizer, ili kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Jumamosi iliyopita wakicheza ugenini katika Uwanja wa FNB (Soccer City), mchezo wa mkondo wa kwanza wa michuano hiyo, Simba walikumbana na kipigo cha mabao 4-0 ambayo yameweka rehani nafasi yao ya kutinga nusu fainali.



Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes ameweka wazi kuwa wataingia katika mchezo wa leo dhidi ya Kaizer Chiefs siyo tu kusaka matokeo ya kufuzu hatua ya nusu fainali, bali wanakwenda kupambana kusaka heshima ya Klabu ya Simba na Watanzania.

 

Gomes alisema: “Tunahitaji kuwa bora hewani, lakini tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunamlinda yule mshambuliaji wao, Samir Nurkovic kwa kuwa ni straika mzuri na mwenye nguvu sana, hivyo ni lazima tutakapokutana tupambane naye kwa nguvu ili kumzuia.
 

 
“Hii ni robo fainali na tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunapindua matokeo, lazima tuuanze mchezo huu kwa nguvu kubwa, Simba siyo tu kwamba inakwenda kutafuta matokeo, bali tunakwenda kusaka heshima ya klabu na Watanzania wote kwa ujumla.

 

GOMES AJA NA MBINU TOFAUTI

Kocha Gomes aliongeza kuwa licha ya kuwa walifanya makosa mengi kwenye mchezo wa kwanza hususan kwenye eneo la ulinzi amesema amejipanga kuyafanyia maboresho na marekebisho makosa waliyofanya ili waweze kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa leo.

 

“Tulifanya makosa mengi kwenye mchezo wa kwanza, hatukuwa bora kwenye mipira ya juu jambo lililosababisha tukaruhusu mabao matatu ya vichwa, nimelifanyia kazi ili kwenye mchezo wa marudio tusiweze kuyarudia, tutaingia na mbinu tofauti kwenye mchezo huo ili tuweze kupata matokeo na kuweza kufuzu hatua inayofuata.”

 

BOCCO MATUMAINI KAMA YOTE

Nahodha wa Simba, John Bocco amefunguka kuwa wao kama wachezaji wamejipanga kuhakikisha wanapambana kwa dakika zote tisini kuhakikisha timu inapata matokeo bora ili waweze kufuzu licha ya mchezo huo kuwa mgumu kutokana na kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao kwenye mchezo wa kwanza.



“Tunaingia kwenye mchezo huu tukiamini kuwa utakuwa mchezo mgumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunapambana kupata matokeo, tulipoteza kwa idadi kubwa ya mabao, tunaamini tunaenda kupambana na kupindua matokeo ili tuweze kusonga mbele.

 

“Sisi kama wachezaji tumedhamiria kupambana kwa dakika zote, ni lazima tujitume tukijua kuwa tulifungwa kwenye mchezo wa kwanza, hivyo ni lazima tupambane kuibuka na ushindi ili kuwapa furaha mashabiki wetu na sisi tuweze kufuzu.”

 

KAIZER WATOA VITISHO

Mara baada ya kutua nchini juzi wakitokea Afrika Kusini, Meneja wa Kaizer Chiefs, Gerald Sibeko alisema kuwa wamejipanga kupata ushindi licha ya ugumu ambao wanaweza kukumbana nao.

 

“Sisi Kaizer Chiefs kutoka Afrika ya Kusini ni moja ya timu bora barani Afrika, tunajikita zaidi kuutazama mchezo wetu dhidi ya Simba, na tunaamini mchezo utakuwa wa kiungwana na taratibu zote za mchezo zitafuatwa, hatuwaogopi Simba kwani malengo yetu ni kufika mbali kwenye michuano hii.



“Tulifanikiwa kuwafunga kwenye mchezo wa kwanza hivyo tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo kwenye mchezo huu ili turudie kile tulichokifanya nyumbani, tupo hapa kuiwakilisha Kaizer Chiefs na Afrika Kusini kwa ujumla, tutajitahidi kadiri ya uwezo wetu ili tuweze kuibuka na ushindi kwenye mchezo huu.”

 

MTOTO WA BOSI KAIZER ATAMBA

Naye mtoto wa mmiliki wa timu hiyo anayefahamika kama Kemiso Moutang, ametamba wataibuka na ushindi leo dhidi ya Simba.

 

“Tunatambua ubora wa Simba wanapokuwa katika uwanja wao wa nyumbani, rekodi zao tunazo na sisi tumejiandaa kuweza kupata ushindi katika mchezo huu licha ya kwamba tupo ugenini.“Malengo yetu ni kufika fainali katika michuano hii, hatuwezi kufikia huko kama tutashindwa kupata ushindi au kufuzu mbele ya Simba tutafanya kila linalowezekana kuyafikia malengo yetu.”

 

Chama la ushindi hili hapa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Joash Onyango, Paschal Wawa, Taddeo Lwanga, Mzamiru Yassin, Bernard Morrison, Clatous Chama, Luis Miquissone, Chris Mugalu.

IMEANDIKWA NA HUSSEIN MSOLEKA, JOEL THOMAS NA MARCO MZUMBE

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad