Dar es Salaam. Usimamizi mbaya wa miradi na kutoshirikisha wanachama katika waamuzi ni miongoni mwa sababu za fedha za wanachama wa Mifuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuwa hatarini kupotea baada ya miradi ya mabilioni kutelekezwa.
Hayo yameelezwa na wadau waliotoa maoni kuhusu kutelekezwa kwa miradi ya nyumba za shirika hilo licha ya uwekezaji mkubwa uliofanyika, hivyo kuibua wasiwasi wa fedha za wanachama kupotea.
Baadhi ya maeneo ambayo miradi ya mabilioni imetelekezwa ni Dege, Dugu, Tuangoma na Mtoni Kijichi jijini Dar es Salaam, ambako miradi imesimamishwa tu kuta za zege na matofali na nyumba nyingine zimekamilika lakini hazikaliwi na watu na mazingira yake yamekuwa vichaka.
Hata hivyo, mfuko huo umesema unakusudia kukamilisha miradi yote na kuifanya izalishe, huku ukibadilisha mwelekeo wa uwekezaji na kulenga miradi yenye faida.
ncccccfpiccc
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia majengo ya mradi wa Dege Eco Village Kigamboni, Dar es Salaam alipotembela mradi huo 2018. Kushoto ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Balozi Ali Siwa na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Azimio, Mohammed Iqbal. Picha na maktaba
Akizungumzia uamuzi huo, Mtaalamu wa uchumi Dk Abel Kinyondo alisema kukamilisha miradi hiyo ni busara kwa kuwa mabilioni ya shilingi za wanachama yalikwishatumika katika miradi hiyo, hivyo kuiacha ni sawa na kupoteza fedha hizo.
“Mabilioni ya fedha za wanachama yamelala hapo na wakati uliopo sasa sio wa kujadili ifanyike au isifanyike na ustaarabu wa kawaida ni kuimalizia ili kuokoa fedha za watu,” alisema Dk Kinyondo.
Aliongeza kuwa ili kuwa na ufanisi ya katika mifuko hiyo ni lazima muundo wa uwekezaji ubadilike na kuwahusisha wanachama zaidi katika maamuzi ya kufanya uwekezaji wa fedha ambazo ni michango yao.
Dk Kinyondo alisema ni vigumu mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ujumla kufanya vizuri katika uwekezaji kama hakuna bodi huru inayowasimamia na miongoni mwa watu wa kuunda bodi hiyo wawe ni wanachama ambao ndiyo wenye fedha.
“Bodi inapaswa kuwa ya kuwasilisha masilahi ya wanachama, ikiundwa na wanachama ambao ndiyo wenye pesa zao, msimamizi anaweza asiwe na masilahi sawa na mwenye mali. Uwekezaji usipoenda vizuri mwanachama anaathirika moja kwa moja tofauti na msimamizi,” alisema Dk Kinyondo.
Alisema bila kujali hata taaluma aliyonayo mwenye mali anaweza kufanya maamuzi yenye maslahi makubwa kwake kuliko msimamizi hivyo mifuko hiyo ya umma inapaswa kufanya kama kampuni zinavyowashirikisha wanahisa wake kwa kuwaeleza jambo ambalo wanakusudia kufanya na kupata Baraka zao.
Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) Said Wamba alisema kinachotakiwa kuongezeka na umakini katika kuamua masuala yanayohusu ustawi wa mfuko na wanachama.
Alisema anaamini katika muundo wa sasa wa kuwa na uwakilishi wa wafanyakazi na wataalamu wengine lakini “Wanaopaswa kulaumiwa kwa yaliyotokea si menejimenti, bali na watu wote wanaohusika kwa kuwa bodi inajumuisha watu tofauti wakiwamo wakilishi wa wafanyakazi, viongozi wa Serikali na wataalamu mbalimbali,” alisema Wamba.
Mkakati mpya
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mushomba amelieleza Mwananchi kuwa ipo miradi ambayo mfuko wenyewe utaimalizia, ambayo watatafuta wabia na mingine wataiuza kwa watakaokuwa tayari.
Katika hatua hiyo, alisema kitakachozingatiwaa ni masilahi ya mfuko na kuhakikisha uamuzi unaofanyika hauleti matokeo hasi. Mushomba alifungua mlango kwa watu wenye nia ya katika miradi ya Dege, Dungu, Tuangoma na Kijichi wawasiliane na mfuko huo ili kuingia makubaliano.
Miradi ya hasara
Pamoja na hayo, Mkurugenzi mkuu alisema mfuko unakusudia kuachana na miradi yote ambayo haina manufaa kwao na maelekezo ya Serikali yanawataka kuwekeza zaidi katika miradi inayolipa.
“Ndani ya kipindi kifupi (bila kukitaja) suala la miradi ya NSSF isiyozalisha litabaki kuwa historia, nguvu itakuwa katika miradi ambayo inaleta ufanisi wa mfuko na usalama wa fedha za wanachama. Ukitufuatilia siku zijazo utagundua kuwa uwekezaji katika nyumba (real estate) utapungua kwa kiwango kikubwa,” alisema.
Alisema mwelekeo wao wa sasa utakuwa zaidi katika kununua hati fungani za Serikali (Treasury Bills na Treasury Bonds) pamoja na kununua hisa katika makampuni ambayo mfuko utaona kuna fursa ya kupata faida kutokana na uwekezaji uliofanywa.
“Kwa sasa tumebadili mwelekeo wetu wa uwekezaji, nguvu yetu itakuwa katika hati fungani ambayo kwa sasa faida yake ni asilimia 15 ambayo ni kubwa kuliko mfumuko wa bei, Vilevile katika ununuaji wa hisa katika kampuni ambazo tunaona tutapata faida,” alisema.
Mushomba alisema Serikali ya sasa imewapa maelekezo madhubuti ya kuhakikisha kuwa wanafanya uwekezaji katika maeneo yanayoleta faida kwa mfuko ambapo faida hiyo inaongeza mapato ya Serikali kupitia kodi lakini pia kutoa ajira kwa watu wengi.
Mradi kama wa Dege ambao ukubwa wake ni ekari 300, kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ya 2016/17 ulisimama ukiwa tayari umegharimu Sh220 bilioni.
Mradi huo ambao mpaka kukamilika kwake ungekuwa na thamani ya Sh1.3 trilioni NSSF iliingia katika ubia na Azimio Housing Estate Limited (AHEL) ikimiliki asilimia 45 na AHEL asilimia 55. Katika ya asilimia 55 za AHEL, asilimia 20 ni thamani ya ardhi.
Mwaka 2016 NSSF ilitoa mradi huo kwa Kampuni ya udalali ya Yono ili kuunadi na fedha ambayo walitarajia kupata ni Dola za Marekani milioni 350 sawa na Sh811.7 bilioni lakini hakupatikana mnunuzi, hata baada ya kukaribisha wawekezaji wadogo wa kuchukua sehemu tu ya mradi.
Mradi wa Dungu una nyumba 439 na umegharimu jumla ya Sh89.5 bilioni ambapo hadi mwa[1]ka 2018 mfuko huo ulikuwa umeshaweka Sh50 bilioni huku mradi wa mradi wa Tuangoma wenye nyumba 161, mpaka 2018 ulikuwa umetumia Sh61 bilioni.
Januari, 2020 NSSF ilitangaza kuwa nyumba zake za Mtoni Kijichi zingetumika kama hosteli za wanafunzi 17,820 wa vyuo vya vikuu vinne vya mkoani Dar es Salaam kwa makubaliano maalumu na vyuo hivyo, hata hivyo mpango huo haukufanikiwa kwa sehemu kubwa.
Vyuo hivyo ni Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA).
Mwananchi