Sumsang Waipiku Apple kwenye Mauzo ya Simu



UAMUZI wa kampuni ya simu ya Samsung kushusha bei ya simu zake aina ya Galaxy S21 unaonekana kuipa faida kampuni hiyo baada ya kumpiku mpinzani wake wa karibu, Apple katika mauzo ya simu duniani kwa robo ya kwanza ya mwaka huu.

 

Kampuni hiyo ya Korea Kusini imeonekana kufanya vizuri katika mauzo ya simu kwa kuteka soko kwa asilimia 22, ikiuza takriban simu milioni 76.5, ikilinganishwa na Apple iliyouza simu milioni 52.4 na kuambulia asilimia 15 tu ya soko kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu.

 

Samsung iliamua kushusha bei ya simu zake za Galaxy S21 kufikia dola 200 (sawa na sh 466,000). Licha ya kushuka kwa mauzo, Apple imeendelea kuingiza kiasi kikubwa cha fedha, ikijitapa kuongezeka kwa mauzo ya iPhone kwa asilimia 65.

 

Tofauti na matarajio, iPhone 12 Mini imeuza chini ya kiwango, lakini aina zingine za simu kama iPhone 12 na iPhone 11 zimeifanya Apple kuendelea kubaki sokoni ndani ya robo hii ya kwanza ya mwaka.

 

Anayefuata kwa karibu ni Xiaomi ya China, ambayo imeuza simu milioni 49 na kufanikiwa kuteka asilimia 14 ya soko. Oppo na Vivo zimebaki katika nafasi tano za juu kwa kuuza simu milioni 37.6 na milioni 36 kila mmoja, wakati Huawei ikiporomoka hadi nafasi ya 7.

 

Kwa ujumla, soko la simu janja limekua kwa asilimia 27 katika robo ya kwanza ya mwaka, ikiuza jumla ya simu milioni 347, ukilinganisha na mwaka jana.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad